Straika wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma,
ameendelea kuwa tishio katika soka la Bongo kutokana na kasi yake ya kucheka na
nyavu, baada ya juzi Jumatano kufunga mabao mawili katika sare ya mabao 2-2
dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga.
Kasi yake imemshtua Kocha Msaidizi wa Mwadui,
Habib Kondo ambaye hakutaka unafiki na kujikuta akimmwagia sifa Mzimbabwe huyo
kwa kusema kuwa ndiye alikuwa kikwazo kikubwa kwao katika mchezo ule kutokana
na soka lake la nguvu na la kibabe, spidi kubwa uwanjani na jamaa hachoki.
Kondo anasema pamoja na kikosi chao kuwa kwenye
ubora mzuri dhidi ya Yanga, bado nyota huyo wa zamani wa FC Platinum, alikuwa
fiti mwanzo-mwisho na kwamba aliitesa safu yao ya ulinzi.
“Yanga ina kikosi bora, wao ndiyo mabingwa lakini
yule Ngoma ndiye alitupa wakati mgumu sana. Jamaa ni msumbufu sana, ana nguvu,
ana kasi ya soka na hachoki. Kwa kifupi ni mpambanaji mzuri na alikuwa kikwazo
kwetu, ingawa timu nzima ilicheza vizuri,” alisema Kondo.
Mabao hayo yalimfanya Ngoma kufikisha mabao saba
katika mechi nane katika Ligi Kuu Bara ikiwa ni msimu wake wa kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment