Na
Saleh Ally
UCHAGUZI Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
bado uko katika mchakato wa hesabu na karibu kila Mtanzania anasubiri kwa hamu
kupata majibu yake.
Kuhusiana na udiwani na ubunge, sehemu
nyingi majibu yamepatikana na kila upande hasa sehemu mbili zenye upinzani CCM
na Chadema, zimeanza kujua mwelekeo.
Kwamba kila upande umeshinda huku,
umeshindwa kule na kinachobaki ni kujipongeza na kusikitika katika sehemu
ambazo wamefeli.
Wakati matokeo yanaendelea kutoka, Kamati ya
Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) imefuta uchaguzi wa visiwani humo kwa madai haukuwa
wa huru na haki na tayari kumekuwa na mijadala kuhusiana na suala hilo kama ni
sahihi au la.
Wako
ambao wamekuwa wakitaka na uchaguzi wa Tanzania Bara kufutwa. Lakini Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (Nec), Jaji Mstaafu, Damian Lubuva amelishafafanua
hilo kwamba ni sehemu mbili ambazo haziingiliani.
Upande wa Bara, nako tayari Chadema kupitia
mgombea wake wa Urais, Edward Lowassa wamesema hawayatambui matokeo
yanayoendelea kutolewa kwa madai hawajatendewa haki. Lakini niwe mkweli,
sikuona kama wana hoja za msingi.
Hali
kadhalika, upande wa CCM ambao mgombea wao wa Urais ni John Pombe Magufuli, nao
wamelalamika kwamba hawakutendewa haki kwenye uchaguzi wa wabunge. Mfano wao
mmoja ni jimbo la Kawe ambalo Halima Mdee wa Chadema amemshinda Kipi Warioba wa
CCM. Wao wameamua kwenda mahakamani.
Haya
ni makala ya michezo kuhusiana na hali ya nchi yetu kwa kuwa sisi wanamichezo
tunaishi ndani ya nchi hii. Nataka niwakumbushe wanasiasa kuwa wazalendo na
kuangalia kwamba wanachotaka kufanya kinaonyesha kina maslahi yao binafsi na si
kwa ajili ya nchi yetu.
Nataka kuwakumbusha kwamba katika ushindani
huu, lazima CCM wangeshinda upande fulani na Chadema kwa upande wa Ukawa
wangeshinda kwingine.
Mkitaka kung’ang’ania mmoja ashinde kila
upande ni jambo ambalo haliwezekani. Pia naona hoja zenu zinazojengwa kwamba
mmeonewa, si kubwa na zinazoeleweka. Zinaonyesha mnataka madaraka tu.
Nimeona vijana wengi mnashiriki, mnaingia
mitaani, mnachoma majengo lakini najua mnafanya hivyo kwa ushawishi na manufaa
ya wanasiasa hao ambao mkiumia wataishia kuwapa pole za midomo na wakifanikiwa
mtawaona wanapita mbali na hata nafasi ya kuwaona kwenu itakuwa shida kabisa.
Chonde vijana wenzangu, tunahitaji amani kwa
kuwa Tanzania ndiyo kwetu, hatuna pa kwenda zaidi ya hapa. Tusiichezee amani
yetu kwa kutaka kumfurahisha Lowassa au Magufuli au kuonyesha tunazipenda sana
Chadema au CCM.
Kwa upande wa wanamichezo niwakumbushe,
kutakapokuwa hakuna amani. Hatuwezi kuona mechi za Ligi Kuu Bara, hatutakuwa na
nafasi ya kushuhudia mechi za England, Hispania au kwingineko Ulaya tukiwa
tumetulia.
Nawakumbusha timu yetu ya taifa, Taifa Stars
ina jukumu kubwa Novemba 14 itakapokuwa inapambana na Algeria kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam. Bila amani, hatutaenda uwanjani na huenda mechi
itahamishiwa Kenya, Rwanda, Burundi au kwingineko ambalo si jambo sahihi.
Bado kumbuka kuna watoto na vijana wengi wa
Kitanzania wanahitaji kukua katika michezo mbalimbali. Ili wafikie ndoto zao
lazima kuwe na viwanja na makocha bora. Lakini amani inahitajika kwa ajili ya
utekelezaji kufikia ndoto zao. Pia michezo, ndiyo inaweza kuwakutanisha nyote
mliofarakiana kama walivyofanya Rwanda na nchi nyingine nyingi. Mnaweza
kuitumia kama sehemu ya umoja.
Siamini kudai haki kwa kubomoa taifa ni
sahihi, siamini kama ushabiki au uroho wa madaraka kwa viongozi wa vyama vyote
vinavyoonesha uchu ni sahihi. Tuangalie nchi yetu, tukumbuke hata walioharibikiwa,
kabla waliishi kwa amani, wakalilia kura na kudai wanaonewa, mwisho wameharibu
nchi zao na leo wanaishi katika nchi za wengine ambao ni wavumilivu.
Kutoka hapa ukaishi nchi yenye amani pia ni
aibu. Kwani unafikiri unakokimbilia wao huwa hawakorofishani au kutofautiana.
Lakini kuna mambo walitumia busara ndiyo maana wakabaki na amani. Tafadhali
wanasiasa, tafadhali WanaCCM, Chadema, Cuf na vyama vingine. Fanyeni yenu,
lakini amani ndiyo muhimu zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment