Katika kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inafunga mabao mengi kwenye mechi, Kocha
Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, ameanza kutengeneza mbinu mbalimbali
zitakazowapa ushindi wa mabao mengi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo, hadi
hivi sasa imefanikiwa kufunga mabao saba pekee katika mechi tano za ligi kuu,
kati ya hayo matano yamefungwa na mtu mmoja, Mganda, Hamis Kiiza. Lakini Ijumaa
iliyopita, Kerr aliamua kuwapa wachezaji wake mazoezi ya kufunga mabao ya
mashuti ya umbali wa mita 20, ili wawe na wigo mpana wa kufunga.
Zikiwa ni siku
mbili kabla ya kusafiri kwenda Mbeya kutafuta pointi sita katika michezo dhidi
ya Mbeya City na Prisons, Muingereza huyo alionekana kuwa bize akiwafundisha
wachezaji wake kufunga mabao ya umbali wa kuanzia mita 18 hadi 20 kwenye
mazoezi yaliyofanyika katika Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam,
yaliyotumia saa mbili kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:00.
Kerr kwa kuanza
mazoezi, aliwataka wachezaji hao kukimbia mbio fupi wakizunguka nusu uwanja
kabla ya kufanya programu ya kupigiana pasi kwa wachezaji wawili na baadaye kuhamia
katika kuwapa mbinu wachezaji wake jinisi ya kufunga mabao.
Kocha huyo
alianza na programu ya kutengeneza mabao kwa kutokea pembeni akiwataka mabeki
wa pembeni, Hassan Kessy, Emily Nimubona na viungo wa pembeni Simon Sserunkuma
na Awadh Juma kuwapigia krosi wachezaji wenzao zilizofika ndani ya mita 18 kwa
ajili ya kufunga mabao.
Wakati mazoezi
hayo yakiendelea, wachezaji wake walionekana wakifanya kwa ufanisi mkubwa kwa
kufunga mabao, akiwemo Msenegali Pape Nd’aw aliyefunga mabao manne, Joseph Kimwaga
matano na Mussa Mgosi matano.
Mara baada ya
kuwapa mbinu za kufunga mabao hayo ya mita 18, alihamia kwenye mabao ya mita 20
akiwatumia viungo kutuliza mipira mirefu iliyopigwa na mabeki kwenye umbali huo
uliowekewa alama za koni kabla ya washambuliaji kupiga mashuti.
Mara baada ya
mazoezi hayo kumalizika, Kerr alisema: “Ndiyo maana leo (juzi) kama ulivyoniona
programu yangu ilikuwa ya kuwapa mbinu mbalimbali za ufungaji mabao katika
mechi kwa njia tofauti ili mechi zijazo tupate ushindi wa mabao mengi kwa
kuanzia mechi na Mbeya City.”
Simba jana
Jumapili asubuhi iliondoka Dar kuelekea Mbeya kwa ajili ya mechi dhidi ya Mbeya
City Jumamosi hii, kabla ya kuivaa Tanzania Prisons Jumatano ijayo.
0 COMMENTS:
Post a Comment