Hatimaye uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa timu ya Toto
African ya Mwanza inayoshiriki Ligi Kuu Bara umefanyika jana Jumapili jijini humo.
Uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, ulikuwa ni wa kumchagua
mwenyekiti pamoja na wajumbe ambapo ulifanyika kwa takriban saa sita huku
ukigubikwa na mvutano mkubwa kutoka kwa wanachama na kamati utendaji ya timu
hiyo.
Godwin Aiko ndiye aliyetangazwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata
kura 37 akimpita mpinzani wake, Octavian Komba aliyepata kura 16.
Kwa upande wa wajumbe ambapo nafasi mbili zilikuwa zikiwaniwa,
Timothi Kilumila alipata kura 52 na Lushingo Lushingo alipata kura 23 na
kuibuka washindi.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Toto African ya jijini Mwanza,
Mjerumani, Martine Grelics, ametamka wazi kuwa, kama vijana wake hawatapewa
fedha wanazodai klabuni hapo, basi hataipeleka timu uwanjani kucheza mechi za
Ligi Kuu Bara.
Mjerumani huyo ametamka hayo ikiwa ni siku chache tu baada ya
wachezaji wa kikosi hicho kugoma kufanya mazoezi kutokana na madai mbalimbali
ya fedha wanazodai klabuni hapo ambazo zinakadiriwa kufikia milioni 12.
Fedha wanazodai wachezaji hao ni za usajili, mishahara na posho za
safari za michezo yao ya nje ya mkoa.
“Vijana wangu bado hawajapewa fedha wanazodai na nimewaambia
viongozi mpaka ikifika Jumatatu (leo) kama hawajapewa basi mimi pamoja na benchi
zima la ufundi hatutasafiri na wachezaji kwenda kucheza mechi zetu jijini
Mtwara dhidi ya Ndanda na ile ya Dar es Salaam dhidi ya Yanga, viongozi
wanapaswa kutatua tatizo hili haraka,” alisema Grelics.
0 COMMENTS:
Post a Comment