Katibu wa Kamati ya Taifa Stars, Teddy Mapunda leo
amefanya makutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF
uliopo Karume, ambapo ametumia nafasi hiyo kutangaza namba za simu za
uchangiaji kwa Watanzania kwa ajili ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Akizungumza na waandishi wa habari, Teddy
amesema watanzania wanaweza kuichangia Taifa Stars kiasi chochote cha fedha
kuanzia shilingi mia moja (TZS 100) kwenda namba 0654-888868 (Tigo
Pesa) na 0789-530668 (Airtel Money) ambazo zitatumika kwa ajili
ya motisha kwa wachezaji, uhamasishaji/masoko na maboresho ya kambi za ndani na
nje ya nchi.
Aidha, Teddy amesema Kamati ya Taifa Stars inaandaa
utaratibu kwa ajili ya washabiki watakaotaka kusafiri kuelekea nchini Algeria
katika mchezo wa marudiano, waweze kuchangia gharama za usafiri ili waweze
kwenda kuipa sapoti Stars katika mchezo wa marudaiano Novemba 17, 2015.
“KamatI inaendelea na mchakato wa kukamilisha suala la
kambi ya Taifa Stars, na mpaka sasa tunasubiri majibu kutoka katika vyama vya
soka vya vya nchi tunazotaka kuweka kambi ambazo ni Afrika Kusini, Dubai na
Oman kabla ya kutangaza rasmi kambi itakapokuwa” Alisema Teddy.
Kamati inawaomba watanzania, wadau, washabiki na
wapenzi wa mpira miguu nchini kuichangia timu ya Taifa kupitia namba
zilizotolewa na pia kujitokeza kwa wingi kuujaza uwanja wa Taifa siku ya mchezo
wa tarehe 14 Novemba, 2015
0 COMMENTS:
Post a Comment