November 27, 2015


 
IKANAGA AKILIWAKILISHA TAIFA...
Na Saleh Ally
KUMEKUWA na lawama chungu mzima kuhusiana na suala la vyombo vya habari kulalia katika mchezo wa soka huku michezo mingine ikisahaulika.


Lawama hizo zinasukumwa kwa wanahabari, mmoja wao mimi kwamba tumejisahau kupindukia na tunachoona kinafanya vema ni soka pekee.

Sijawahi kukataa kwa asilimia mia kwamba kweli hapo kuna tatizo kidogo kwa upande wa wanahabari kujisahau na huenda malezi ya uandishi, hasa kwa sisi ambao tunapata nafasi ya kufunza wengine, lazima tusisitize kuendelea kuijali michezo mingine.

Wakati sisi tunajitahidi kuwafundisha waandishi wengine, kuwakumbusha pia wengine, basi huenda uwe wakati wa wahusika wa michezo mingine nao kuamka na kuacha mambo mengi wanayoendelea nayo katika kipindi hiki.

Ningependa nitumie zaidi mfano wa mchezo wa riadha ambao katika miaka ya 1970, 1980 na mwanzoni mwa 1990 ulijenga heshima kubwa kwa taifa letu kupitia wanariadha mbalimbali kama Juma Ikangaa, Filbert Bayi na wengineo.

Majina yao sasa ni makubwa katika nchi nyingi, mfano Juma Ikangaa, nimeelezwa hadi wamefikia kuupa mtaa jina lake kutokana na heshima.

Ikangaa ameshinda au kufanya mashindano kibao kama New York Marathon, Boston Marathon, Tokyo Marathon na mengineyo na alifanya hivyo kwa uwezo wake na nidhamu ya juu kabisa.

Lakini niwaulize watu wa riadha, kabla ya kuanza kulaumu wanahabari, sasa wanamtumiaje mtu kama Ikangaa ambaye huenda Japan au Marekani wangependa kuwa naye kwa ajili ya kuwaendeleza tu vijana wao.

Niwaulize tena, wamewahi kumuenzi vipi mtu kama Ikangaa? Serikali, imemsahau, watu wa riadha wamemsahau na sasa badala ya riadha, migogoro ni kibao, kila kukicha ni majungu.

Sasa mnataka kuripotiwa nini zaidi ya migogoro na utumbo ambao hauna lengo la kuendeleza michezo na badala yake malumbano na watu kutaka kushibisha matumbo yao?

Kina Ikangaa na Bayi wapo, hawatumiki lakini angalia mtu kama Selemani Nyambui, ameondoka nchini kwa mara nyingine na safari hii amekwenda kufundisha Brunei.
 
FILBERT BAYI (NAMBA 376) AKIPAMBANA KATIKA MOJA YA MASHINDANO YA KIMATAIFA.

Wakati akiwa hapa, karibu alipokuwa akisikika basi ilikuwa ni malumbano tu kwa kuwa ni kiongozi wa chama cha riadha. Leo anaendeleza au kukuza vijana wa nchi nyingine ambazo zinajua umuhimu wa kuwakuza na kuwaendeleza vijana.

Ikangaa hata angekuwa mshauri bado ingekuwa ni jambo zuri kwa riadha nchini kwa kuwa pamoja na ubora wa kazi yake akiwa mwanariadha lakini ni askari wa jeshi mstaafu.

Wote tunajua nidhamu ya jeshi, Ikangaa amefikia moja ya vyeo vya juu na hiyo ni sehemu ya kuonyesha kiasi gani alikubalika na kupewa heshima kicheo. Cheo kinapatikana kwa heshima kiutendaji.

Utendaji wake lazima ulikuwa bora, ndiyo maana hadi anastaafu aliendelea kuwa mmoja wa askari waliokubalika. Achana na hivyo, Ikangaa kielimu pia ana elimu nzuri, ni mtu aliyekwenda shule.
 
MNYAMBUI (KUSHOTO) AKIBADILISHANA MAWAZO NA IKANGAA.
Angalia hapa, kipaji chake, nidhamu, elimu nzuri lakini bado watu wa riadha hawaoni kama wanaweza kumtumia kuusaidia mchezo wa riadha na badala yake kinachoangaliwa ni hofu kwamba akiwa karibu huenda atakuwa mkali na wengine watashindwa kupata nafasi ya ‘kupiga’ na kujifaidisha.

Watanzania tuna tabia ya kuwahofia watu wenye nidhamu katika kazi au watu wanaopeleka mambo katika mpangilio unaotakiwa.

Tanzania tunawahofia watu ambao ni wachapakazi kwa kuwa tunajua watatuumbua na kuonyesha rundo la upungufu tunaokuwa nao.

Ikangaa mkimpa matofali kujenga ukuta bora wa riadha, kamwe hamhitaji hata kumueleza mnataka nini. Huenda yeye ndiye atawafundisha zaidi nini cha kufanya.

Huu ndiyo wakati sasa, acheni kulialia kwamba hamuandikwi, hamtangazwi au kuonekana kwenye runinga. Pigeni moyo konde mbadili gia angani na watu kama Ikangaa, Bayi na wengine, watumike vizuri kuusaidia mchezo wa riadha ili ukiripotiwa, basi mafanikio yawepo na si kama sasa, majungu kibaooo.


TAFADHARI NI-FOLLOW(Instagram; salehjembe. Twitter; salehjembe)

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic