AME ALI (KUSHOTO) |
Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza, Stewart Hall,
amewawekea ngumu Coastal Union baada ya timu hiyo kupiga hodi klabuni hapo
ikihitaji wachezaji kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Awali, Azam ilitangaza huenda ingewatoa kwa mkopo
baadhi ya nyota wao kwenye dirisha hili la usajili ndipo Coastal ikatumia
mwanya huo kwenda kuzungumza nao mapema ili iwapatie wachezaji hao.
Baadhi ya wachezaji waliotarajiwa kutolewa kwa mkopo
ni Ramadhani Singano ‘Messi’ na Ame Ally, lakini kwa sasa mpango huo
umesitishwa na Hall kwa kusema katika kikosi chake hakuna mchezaji atakayetoka
kwa muda huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Coastal, Salim
Bawazir, amesema wanasikitika kwa dili lao hilo kukwama kwani walipanga
kuwachukua wachezaji hao ili kuziba nafasi kwenye kikosi chao ambapo wanahitaji
kiungo, straika na beki.
“Baada ya kusikia kwamba Azam inataka kuwatoa kwa
mkopo baadhi ya wachezaji wao tukaenda kuzungumza nao, lakini kocha wao mkuu
akagoma kwa kusema wachezaji wote waliopo anawahitaji.
“Kutokana na kauli hiyo, tukawa hatuna jinsi, tukaamua
kwenda sehemu nyingine na tayari kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya
timu ili kuhakikisha kipindi hiki cha usajili tunafanikisha kile
tulichodhamiria,” alisema Bawazir.
Timu ya Coastal mpaka Ligi Kuu Bara inasimama ilikuwa
inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi kumi,
ikishinda moja, sare nne na kupoteza tano.
0 COMMENTS:
Post a Comment