November 18, 2015


Na Saleh Ally
UONGOZI wa Simba sasa unahaha kuhakikisha unapata mshambuliajia wa uhakika ambaye anaweza akaongeza kasi ya ushambuliaji katika kikosi chake.


Simba wanahaha baada ya kufanya makosa makubwa mara mbili ndani ya misimu miwili mfululizo.

Msimu wa 2014-15 walianza kufanya kosa kwa kumuacha mshambuliaji Amissi Tambwe aliyekuwa mfungaji bora msimu mmoja nyuma kwa madai hafai katika mfumo wa Kocha Patrick Phiri. Msimu uliofuata wakamuacha Elius Maguri kwa sababu hiyohiyo, safari hii hafai katika mfumo wa Kocha Dylan Kerr.

Sasa Simba inatafuta mshambuliaji mkali, tena ikiwezekana kwa gharama yoyote na gumzo au anayeonekana kufuatiliwa sana na Mrundi, Laudit Mavugo ambaye Simba ilimkosa kabla ya kuanza msimu, inawezekana ikamalizana naye wakati wa dirisha dogo.

Wakati gumzo la Mavugo linazidi kupambana moto, kuna maswali kadhaa ya kujiuliza ambayo Simba lazima yaingie kwenye ubongo wao kabla ya kuchukua muamuzi wa kumsajili.

Kwanza niwakumbushe, wakati walipovurunda mara mbili kwa kuwaacha Tambwe na Maguri, pia walivurunda kwa kuwasajili Simon Sserunkuma pia Pape N’daw ambao hakika hawana kitu na wamekuwa mzigo, tena afadhari ya wachezaji wazalendo kuliko wageni hao wanaolipwa kwa dola.

Sasa wanataka kusajili, wamejiuliza maswali ya msingi kuhusiana na wanaotaka kuwasajili kama kweli wanauamini uwezo wake au hadithi zimekuwa nyingi hadi zimewashawishi wahakikishe wanampata.

Mimi nimeanza kupata hofu kuhusiana na uwezo wa Mavugo kama kweli ni mchezaji sahihi na ana uwezo wa kuitoa Simba ilipo kwenda mbele, nitakueleza kwa nini.

Wakati Tanzania inapambana na Algeria kuwania kufuzu Kombe la Dunia. Burundi ilikuwa ikipambana na jirani zake DR Congo.

MEchi ya kwanza ilikuwa mjini Bujumbura, wenyeji wakalala kwa mabao 3-2 huku Cedric Amissi akifunga mabao mawili ya Burundi. Wakati huo Mavugo, alikuwa benchi kama ilivyo kwa Amissi Tambwe na Didier Kavumbagu.

Katika mechi iliyofuata, timu hizo ziliporudiana mechi ilikuwa ngumu na matokeo yakawa 2-2. Lakini siku hiyo, kocha aliamua kuwaingiza Tambwe na Kavumbagu kukisaidia kikosi chake kipata angalau bao moja, ilishindikana.

Hii ilikuwa ni mara ya pili, Mavugo anamaliza dakika 90 akiwa benchi. Maana yake mechi mbili amebaki benchi. Kwa sayansi ya soka na filosofia ya kocha wa Burundi inasema Tambwe na Kavumbagu ni bora zaidi ya Mavugo.

Tambwe na Kavumbagu walitumika wakati Burundi ina wakati mgumu na ilitaka bao la tatu, ikiwezekana la nne. Hawa waliaminiwa na mwalimu kuiinua timu kutoka katika hali ngumu.
Kama Mavugo angekuwa hatari, basi angeanza. Kama angekuwa tishio basi angepewa nafasi ya kuikomboa Burundi. Kubaki katika benchi dakika zote 90, mara mbili. Mimi najiuliza hivi, Kavumbagu na Tambwe ni zaidi ya Mavugo?

Kama itakuwa ni sahihi kuwa kweli washambuliaji hao wa Azam FC na Yanga ni wakali kuliko Mavugo. Je, Simba inastahili kuhangaika kumpata kwa gharama yoyote?

Maana hata Tambwe alionekana hafai, vipi isajili mchezaji anayewekwa benchi na Tambwe? Au inaamini ina mwalimu anayeweza kumbadili Mavugo na kuwa hatari zaidi?

Tunaweza kuwaachia Simba wafanye wanalotaka ingawa niwe wa kwanza kuweka hofu yangu mapema kupitia kipimo hicho cha timu ya taifa.
Nitawakumbusha wakati Simba inamsajili Tambwe alikuwa ametokea kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kagame. Yeye ndiye alikuwa mfungaji bora Afrika Mashariki na Kati. Hata baada ya kutua Simba, ingawa kikosi kilikuwa kinasuasua, akaonyesha kweli yeye ni mkali na akaweza kuibuka mfungaji bora.

Sasa kwa Mavugo kuna hivyo vigezo vya ushawishi wa mahesabu na si hadithi? Pia nahoji kama Simba inatumia watu sahihi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kiusajili kuliko kuangalia au kutumia watu wenye wiki mbili tatu katika soka?

Ushauri wangu, kuna kila sababu ya Simba kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kina. Na kama kuna upungufu imeukubali, iwe imejiandaa kukabiriana nao. La sivyo, Simba lazima iamini washambulizi hatari ni wengi mno kikubwa ni kufanya upembuzi yakinifu kwa wigo mpana, kuliko kulazimisha, itakuwa yaleyale.






2 COMMENTS:

  1. analysis ya mavugo sijaikubali sana kwani hata Tz mambo kama haya yapo ....huenda ni kweli lakini pia huenda pia kocha akamweka mchezaji benchi kwa matakwa fulani fulani

    hao hao simba wamemwacha maguli sababu kocha kaona hafai na amekua lulu stand united so analysi hii ni food for thought

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic