Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi,
ametamka kuwa juzi Jumamosi Taifa Stars ilikuwa na uwezo wa kuifunga Algeria mabao
5-0 katika kipindi cha kwanza pekee.
Pluijm ambaye alikuwepo Uwanja wa Taifa jijini Dar, aliishuhudia
Stars ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Algeria kwenye mchezo wa kwanza wa
kusaka nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Stars ilikuwa mbele kwa bao
1-0 huku ikiongeza lingine kipindi cha pili dakika ya 54, lakini ikaruhusu
kufungwa mabao mawili ya harakaharaka dakika za 71 na 74.
Pluijm amesema kama Stars
ingezitumia nafasi ilizozipata kipindi cha kwanza, basi ingeenda mapumziko
ikiongoza 5-0, lakini ilishindwa kuzitumia na kupata bao moja pekee.
Aliongeza kuwa, safu ya ulinzi ya Stars ilipoteza muelekeo kipindi
cha pili huku akimtaja beki wake wa kushoto Haji Mwinyi kushindwa kucheza kwa
umakini na kuruhusu mabao mawili ya harakaharaka.
“Katika kipindi cha kwanza, Stars ilikuwa na uwezo wa kushinda
mabao 5-0, lakini walishindwa kuzitumia, waliporudi kipindi cha pili, mabeki
wao walipoteza umakini na kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara na hatimaye
Algeria ikasawazisha.
“Haji alishindwa kulinda vizuri kwenye upande wake na ukichanganya
na kutokuwa na mawasiliano sahihi kwa mabeki wote, wakashindwa kulinda ushindi
wao, kiukweli inaumiza.
“Lakini Stars inayo nafasi ya kufuzu hatua inayofuata kama tu ikitumia
vilivyo makosa ya Algeria, kwani nimeona mabeki wao hawana spidi, hivyo
washambuliaji wanapaswa kutumia upungufu huo, lakini wawe makini na
washambuliaji wao kwani ni hatari sana,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment