November 20, 2015


Uongozi wa Klabu ya Simba umesema haupaswi kulaumiana baada ya kuona mafanikio ya straika wao wa zamani, Elias Maguri, bali unatakiwa kukaa chini na kumsifia.


Simba ilimuacha Maguri katika usajili wa dirisha kubwa kabla ya kuanza kwa msimu huu, ambapo katika mkataba wa miaka miwili aliosaini akitokea Ruvu Shooting msimu uliopita, ulikuwa umebaki mwaka mmoja.

Straika huyo ambaye ndiye kinara wa kuzifumania nyavu kwenye Ligi Kuu Bara mpaka sasa, anaitumikia Stand United na ameonyesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha Taifa Stars.

Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Simba, Said Tully, amesema hakuna haja ya kuanza kutupiana lawama kutokana na mafanikio ya Maguri, bali kama wanamichezo wanapaswa kumpongeza kwa kufanikiwa kwake kwani wapo wengi walioachwa na klabu kongwe za hapa nchini za Simba na Yanga kisha wakashindwa kuwika huko waendako.

“Maguri tulikuwa naye, kocha wetu mkuu (Dylan Kerr) alimuona lakini nadhani hakuendana na mfumo wake, binafsi naweza kusema badala ya kurusha lawama kwa kocha mkuu au kwa kiongozi yeyote wa Simba, tunapaswa kumsifia kwa kile anachokifanya kwa sasa.

“Nasema hivyo kwa kuwa tumeshuhudia wachezaji wengi wakiachwa na Simba na Yanga na mwisho wake wanashindwa kuwika waendako.

“Maguri anaonekana ni mchezaji mzuri lakini katika kikosi cha Simba hakuweza kuendana na mfumo wa kocha, si kiongozi wala kocha anayepaswa kulaumiwa,” alisema Tully.

Wakati huohuo, katika kile kinachoonekana kuanza kukubali uhalisia kuwa mchezaji huyo anaweza kuondoka klabuni kwake, baada ya kudaiwa kuwa Maguri amefanya mazungumzo na uongozi wa TP Mazembe ya DR Congo ambao unadaiwa kutaka kumsajili, benchi la ufundi la timu yake hiyo  limeanza mchakato wa kusaka mbadala wake.

Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Stand linaloongozwa na Mfaransa, Patrick Liewig, limeanza harakati za kutafuta mbadala wa Maguri.


Kocha msaidizi wa Stand, Athuman Bilali ‘Bilo’, amesema: “Mchakato huo tumeuanza muda si mrefu na ni matumaini yetu kuwa tutampata mrithi wake bila ya tatizo lolote lakini pia tunamuombea kwa Mungu mpango huo wa TP Mazembe uweze kutimia.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic