Uongozi wa Simba umetangaza kuchoshwa na “keshokesho” ya klabu ya Etoile du Sahel katika suala la malipo ya fedha zake, dola 300,000 zaidi ya Sh milioni 630.
Fedha hizo ni za malipo ya manunuzi ya mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyeuzwa kwa klabu hiyo ya Tunisia miaka mitatu iliyopita.
Okwi aliuzwa kwa malikauli na aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ambaye alilaumiwa kwa kutokuwa na mkataba unaowabana Waarabu hao walioonyesha wazi kuwa na nia ya kutapeli Simba.
Lakini uongozi wa Evans Aveva uliingia vitani na kufikia kushitaki kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ambalo liliamuru Etoile kulipa fedha hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo, Aveva amesema wamechoshwa na mambo ya Etoile kuomba wasogezewe mbele suala hilo la malipo.
“Na sisi tumechoka, kila unapofika wakati wa kulipa wanaandika tena barua Fifa kuomba waongezewe muda. Sasa tunataka suala hili liishe kwa kulipwa fedha zetu,” alisema Aveva.
Wakati Etoile ilipotua nchini kucheza na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika, viongozi wake wa juu kabisa waliwaambia waandishi kwamba hawakuwa na sababu ya kulipa kwa kuwa Okwi tayari alikuwa amerejea nchini na anaichezea Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment