December 13, 2015


Na Saleh Ally
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe huenda ni mmoja wa wadau wa soka nchini wenye moyo ulio wazi, walio tayari kusema ukweli bila ya woga na wasio na kinyongo.

Hans Poppe ni mmoja wa wadau wa soka ambao kama kuna kosa, hatasita kusema, lakini kama kuna sehemu ya kusifia, hata kama ni wapinzani, basi ataweka wazi sifa zao nzuri na kuwapongeza.

Kiongozi huyo amesema Simba imekuwa katika wakati mgumu katika usajili hadi kufikia kuonekana inasajili wachezaji wasio sahihi, lakini ukweli ni kwamba Simba haina fedha za kutosha kusajili mchezaji inayemtaka kutokana na mahitaji.

Hans Poppe amesema kipindi hiki, Simba si ile ya miaka kadhaa iliyopita ambayo iliweza kufanikiwa hadi kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek ya Misri.


Kiongozi huyo mwenye ushawishi katika uongozi wa Klabu ya Simba na ‘mshikaji’ au mtani namba moja wa mashabiki wa Yanga amesema anaamini kabisa Simba haina nguvu kifedha kama ilivyokuwa wakati huo.

SALEHJEMBE: Kipi kilichokuwa kinaisaidia Simba hadi sasa kisiwezekana?
Hans Poppe: Unajua watu wanashindwa kutofautisha wakati ule Simba ilikuwa na Mohammed Dewji, sasa Azam FC wana Bakhresa, Yanga wana Yusuf Manji. Hii ndiyo tofauti yake.

SALEHJEMBE: Labda unaweza kuifafanua zaidi?
Hans Poppe: Wakati huo, angalau Simba ingeweza kusajili mchezaji hasa inayemtaka kutokana na uwezo wa juu kifedha. Mo (Dewji) kama mfadhili angetoa fedha kiasi kinachotakiwa. Lakini sasa unaona, Yanga, Manji aliyekuwa mdhamini ndiyo mwenyekiti na atalipa usajili na mambo mengine. Hali kadhalika, Azam FC pia wanahudumiwa na Bakhresa ambayo kampuni yake ni kubwa na tajiri zaidi.


SALEHJEMBE:Nini kinawashinda Simba, kwani inajiendesha vipi?
Hans Poppe: Simba inajiendesha kupitia mapato ya klabu kama viingilio, fedha kidogo za wadhamini pia baadhi ya miradi kama push mobile, uuzwaji wa jezi na kadhalika.



SALEHJEMBE: Sasa vyote hivyo havitoshi kuipa Simba kila inachotaka hasa wakati wa usajili?
Hans Poppe: Unaona tunasajili wachezaji, lakini hatuwezi kuwa na fedha kama dola 250,000 (zaidi ya Sh milioni 525) kumsajili Ngoma kwa kuwa fedha yetu kwa maana ya kipato hairuhusu, lakini tunashukuru, bado si ombaomba au hatumpigii mtu magoti na tunaendelea.


SALEHJEMBE:Unaposema hamumpigii magoti, una maanisha nini? Nani amewahi kupiga magoti?
Hans Poppe: Wako ambao mtu mmoja akitaka kuondoka, wanapiga magoti. Umeona Yanga wakifanya hivyo kila wanaposikia Manji anataka kuondoka. Simba ni tofauti, timu inajitegemea na hakuna mtu mmoja anayeonekana akiondoka kuwa itakwama.


SALEHJEMBE: Kuna taarifa Simba ina mgogoro wa ndani kwa ndani, kwa nini msiachane nao ili kuijenga vizuri timu yenu ambayo mnatumia fedha kuisajili?

Hans Poppe: Nikuhakikishie hakuna mgogoro kama inavyoelezwa, kwamba kuna mtu anataka kuhujumu timu. Ila kuna klabu moja kongwe imetenga Sh milioni 15 kutuhujumu, tunajua kila kitu na tunatoa onyo kabisa. Si sahihi na vema kuwe na ushindani sahihi.



SALEHJEMBE: Waswahili wanasema lisemwalo lipo…
Hans Poppe: Kweli, lakini hili jambo haliko hivyo. Ndiyo maana tumekaa kimya tu kwa kuwa tunajua kila kitu na Jumatatu iliyopita, hao watu walikutana na kutujadili wakati hata hawachezi na sisi. Kisa wanataka kutuhujumu tu ili wapunguze ushindani.

SALEHJEMBE: Kipi mmeamua kufanya?
Hans Poppe: Tunajua, tutapambana hadi mwisho na siku moja tutawaanika. Kikubwa waamuzi wachezeshe kwa haki mechi zetu ili kuwe na uhakika wa maana ya ushindani.


SALEHJEMBE:Vipi kuhusu Kocha Kerr, anakwenda vizuri lakini mnataka kumfukuza, tatizo nini?
Hans Poppe: Nafikiri ni maneno tu, vitu vingi vya Simba vinazushwa sana. Msimu uliopita tulitoa sare mfululizo. Huyu kocha sasa kashinda mechi saba na sare mbili, unawezaje kumfukuza? Kwa kifupi tupo naye na anaendelea kama unavyomuona, tunachoangalia ni mbele.


SALEHJEMBE: Tukirudi katika usajili, kama mwenyekiti umeridhika?
Hans Poppe: Kwa marekebisho tuliyotaka kufanya, hakuna tatizo labda tusubiri uwajibikaji uwanjani.


SALEHJEMBE: Nimeuliza umeridhika?
Hans Poppe: Kwa tulicholenga, nimeridhika. Tulianza na ushambulizi kwanza na tumemrudisha (Paul) Kiongera, tumemchukua (Brian) Majegwa, usisahau tuna (Danny) Lyanga. Pia kuna bwana mdogo hatari tu anaitwa (Hija) Ugando na beki mmoja (Novatus Lufunga), nafikiri inatosha kabisa. Kikubwa watu wajitume tu.

SALEHJEMBE:Taarifa za kuwa mnarudisha Emmanuel Okwi, vipi anakuja lini?
Hans Poppe: Kweli tulipata taarifa za kwamba wanataka kumuuza, tukafanya mazungumzo nao. Wakati fulani nilisafiri kwenda China, baadaye nikaenda Ujerumani na Uholanzi. Nikiwa Amsterdam nilifanya mazungumzo marefu na Okwi, akakubali kurudi.

SALEHJEMBE:Mwisho wake imekuwaje?
Hans Poppe: Naona tutashindwa, maana mwanzo walisema wanamrudisha kwa fedha zile tulizowauiza, tulikubali kulipa taratibu, yeye Okwi tukakubaliana naye. Lakini sasa naona wamebadilika na kuongeza bei.

SALEHJEMBE:Wanasemaje?
Hans Poppe: Wanataka hadi dola 440,000  (Sh milioni 924), hatutaweza. Acha tuendelee na hawa tulionao kwa kuwa tunawaamini na imani kubwa ipo kuwa watafanya vizuri tu.


MARA YA KWANZA, MAKALA HAYA YALIANDIKWA KWENYE GAZETI LA CHAMPIONI, JANA.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic