January 1, 2016




Na Saleh Ally
JUZI Jumatano, Mbwana Ally Samatta alielezea namna ambavyo alicheza mechi yake ya kwanza TP Mazembe na kufanikiwa kufunga bao lake la kwanza kabisa.

Alisimulia kuhusiana na kusimamishwa kwa Tresor Mputu aliyekuwa nyota na nahodha wa TP Mazembe. Baadaye aliporejea, Samatta akahama namba lakini alimsaidia kufanya vema kutokana na kumpa pasi nyingi za mabao.

Swali la mwisho aliloulizwa Samatta lilihusiana na kuhusiana na mazoezi ya ziada ambayo alieleza ilikuwa ni lazima ayafanye kujiweka fiti zaidi kiushindani.

SALEHJEMBE: Unapozungumzia mazoezi ya ziada, kwa kijana wa Kitanzania anayetaka kuwa kama wewe, unamfafanuliaje au yanakuwaje na kwa kipindi kipi?
Samatta: Ni kujituma zaidi, kufanya mazoezi ya ziada nje ya yale ya kocha au kikosi kwa pamoja. Kama kwa siku tutafanya mara moja, mimi lazima nifanye mara nyingine.

Mfano kama tunafanya asubuhi, basi mimi ntafanya jioni, ikiwa jioni, mimi ntafanya asubuhi. Inaweza kuwa barabarani kutafuta upepo (pumzi), gym au uwanjani, inategemea. Unajua mnapokuwa kwenye ligi, mwalimu anakuwa anaamini mpo fiti, hivyo mnafanya mazoezi kidogo sana. Sasa mimi najiongeza.

SALEHJEMBE: Vipi maisha kama staa katika nchi ya ugenini kama Congo, unaishi kwa raha, hakuna shida kutoka kwa mashabiki?
Samatta: Mashabiki wa Congo kidogo wana tofauti na wa hapa nyumbani. Utaona kuna wachezaji wengine wamekuwa na walinzi wanatembea nao, mimi kidogo tofauti. Nikiamua kutoka nakwenda tu, nazungumza nao halafu naendelea na shughuli zangu na wananielewa kabisa.

SALEHJEMBE:Umesema mashabiki wa Congo wana tofauti na wa hapa nyumbani, kivipi?
Samatta: Kule Congo, mashabiki wakikupenda hawawezi kuficha, wanachanganyikiwa kabisa. Hapa nyumbani ni tofauti kidogo, shabiki anaweza kuwa anavutiwa na wewe ila kukitoa hicho kitu akuonyeshe hawezi, anabaki nacho moyoni.

SALEHJEMBE:Vipi ujio wa Ulimwengu kujiunga na TP Mazembe, ulikusaidia lolote?
Samatta: Niseme ulinisaidia sana, pia ulimsaidia sana Ulimwengu.

SALEHJEMBE: Iliwasaidia kivipi, kwa kiasi gani?
Samatta: Baada ya kuja kwa Ulimwengu, nilipata mtu ambaye tunaweza kupiga stori nyingi na wakati mwingine kujisikia kama niko nyumbani. Haina maana wengine sikuwa nikizungumza nao, lakini mtu wa nyumbani ni nyumbani tu.

SALEHJEMBE:Mlikuwa mkipata nafasi ya kushauriana kuhusiana na maisha?
Samatta: Ndiyo, kwanza nikuambie Ulimwengu kwa sasa ni kama ndugu yangu, tunashauriana mambo mengi sana tena sana. Nikukumbushe, urafiki wangu na Uli haukuanzisha TP Mazembe, tulicheza pamoja timu ya taifa chini ya miaka 20, tulikuwa marafiki wazuri tu.

SALEHJEMBE:Taifa Stars ilikutana na kipigo kibaya kabisa cha mabao 7-0 mkiwa uwanjani. Ulifanikiwa kupata hisia kabla kwamba mambo yangekuwa mabaya hivyo?
Samatta: Sidhani kama kuna aliyewaza hivyo, nilijua mechi ingekuwa ngumu sana dhidi ya Algeria, lakini sikufikiria suala la mabao saba.

SALEHJEMBE: Nini ulifikiri baada ya mechi ya Dar es Salaam ambayo iliisha kwa sare ya 2-2 huku Tanzania ikipoteza nafasi nyingi za kufunga?
Samatta: Nilianza kuamini tungeweza kufanya vizuri, nilijua mechi ni ngumu lakini pia wanaweza kufungika.

SALEHJEMBE: Baada ya kipigo cha mabao saba, usiku wake hali yako ilikuwaje?
Samatta: Nilikuwa sijielewi kabisa. Wakati mwingine nilicheka bila ya kujijua, wakati mwingine nilishangaa, sikujua kipi ni sahihi.

SALEHJEMBE: Hukujielewa, kuna chochote ulifanya ambacho si cha kawaida?
Samatta: Hapana, niliamua kumuita Uli, nikamuambia aisee hawa jamaa ndiyo profesheno kweli.

SALEHJEMBE: Kwa nini ulimuambia hivyo?
Samatta:… 



USIKOSE SEHEMU NYINGINE KESHO JUMAMOSI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic