Unaweza ukadhani ni utani lakini ukweli ni kwamba nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisahaulika katika upigaji kura kumchagua Mchezaji Bora wa Dunia ‘Ballon d’Or’ iliyotwaliwa na Lionel Messi wa Barcelona juzi Jumatatu.
Kwa mujibu wa taratibu, kura hizo hupigwa na nahodha na kocha wa timu ya taifa pamoja na ofisa habari wa shirikisho la nchi husika, lakini kwa Tanzania, Cannavaro yake ilipotea bure kwa kushindwa kutimiza haki yake kidemokrasia kwa kile alichosema hakuambiwa kuwepo kwa mchakato huo.
Messi alitwaa tuzo hiyo kwa kuwabwaga Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Neymar dos Santos wa Barcelona ambao waliingia kwenye Tatu Bora, ikiwa ni tuzo ya tano kwa staa huyo raia wa Argentina.
Hata hivyo, kuna ukakasi kuhusiana na kura ya Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ambaye amesema alipiga lakini haionekani kwenye mtandao wa Shirikisho la Soka Tanzania (Fifa).
Katika orodha iliyotolewa na Fifa, ni Boniface Wambura (Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi) ndiye pekee kutoka Tanzania ambaye kura yake imeonekana kwenye mtandao, huku kura za ofisa habari (Baraka Kizuguto) na Mkwasa zikiwa hazionekani.
Alipotafutwa Wambura kuhusu jina lake kuonekana kwenye mtandao ya waliopiga kura wakati si ofisa habari tena, alisema: “Mimi nimeanza kupiga kura hata kabla sijawa ofisa habari wa TFF, nilichaguliwa na Jarida la Michezo la Ufaransa kama mwandishi mwakilishi kutoka Tanzania katika upigaji kura, hivyo mimi ninaendelea kupiga tu.”
Mtandao wa Fifa unaonyesha kuwa Wambura alimpa kura Ronaldo, wakati hiyo ya Mkwasa ambayo haionekani anasema alimpa Messi.
“Sikupigiwa simu kupewa maelekezo ndiyo maana sikupiga kura, lakini kama ningeambiwa basi ningepiga,” alisema Cannavaro.
0 COMMENTS:
Post a Comment