Na Saleh Ally
MECHI ya Simba na Yanga ndiyo kubwa zaidi ya watani wa jadi katika ukanda wa Afrika Mashariki hilo haliwezi kuwa na ubishi.
Lakini kama utazungumzia ukanda wa kati, kuna mechi mbili; moja ni AS Vita na TP Motema Pembe ndani ya DR Congo. Halafu ile ya APR dhidi ya Rayon Sports pale jijini Kigali Rwanda.
Hizo nazo zina msisimko mkubwa, ingawa Simba dhidi ya Yanga zinaendelea kubaki gumzo na mechi yenye mashamsham ya aina yake, pia hilo hali ubishi.
Mechi inayowakutanisha hao watani wawili, Yanga na Simba ina mengi kabla, ina mengi siku ya mechi uwanjani. Lakini ikiisha pia, mambo kibao huendelea kutokana na ukubwa wake.
Si rahisi kuingia mechi nyingine katikati ikaiangusha hiyo. Lakini lazima tukubali katika ulimwengu wa sasa hakuna kinachoshindikana. Anayeonekana mdogo, kama atalala basi iko siku itafikia, atakuwa mdogo.
Umaarufu wa mechi ya Yanga dhidi ya Simba nchini ni namba moja. Mechi inayoshika umaarufu sasa ni pale Azam FC inakupokutana na Yanga, iwe inachezwa Tanzania Bara au Visiwani, ushindani ni uleule, presha ni kubwa na hakuna anayekubali kufungwa.
Taratibu inaonekana mechi hiyo inazidi kuchukua umaarufu. Tayari imechukua ule umaarufu wa Yanga inapokutana na Coastal Union au Simba inapoivaa African Sports ya Tanga pia.
Baada ya Yanga kucheza na Simba, basi wengi husubiri Yanga ikutane na Azam FC. Baada ya hapo, mechi itakayofuatia kwa umaarufu ni ile Azam FC inapokutana na Simba.
Utagundua, timu inayotengeneza mechi kubwa ya pili na ya tatu ni Azam FC ambayo imezaliwa mwaka 2004 tu. Huku ile ya kwanza kwa ukubwa inayowakutanisha Yanga na Simba, historia yake inaanzia mwaka 1935 kwenda 36 hadi leo hii.
Hisia za dharau au kutoamini mapema, zimewaangusha watu wengi sana katika mambo mengi sana pia. Inawezekana hakuna anayeona inawezekana mechi ya Yanga na Azam FC ikawa kubwa kuliko zote hapa nchini.
Kwa kuwa historia ya Yanga dhidi ya Simba ni ndefu, inahusisha uhuru, wazee na asili ya timu zenyewe. Lakini inawezekana kabisa wakati mechi ya vigogo hao ikibaki kuwa mechi kubwa kwa historia, mechi ya Yanga dhidi ya Azam FC inaweza kuchukua nafasi ya kuwa mechi “maarufu na yenye mvuto zaidi” Tanzania.
Simba dhidi ya Yanga zikabaki kuwa mechi kubwa zaidi. Halafu Yanga dhidi ya Azam ikachukua sifa hiyo ya mechi yenye mvuto na maarufu na watu wakaendelea kuisubiri kwa hamu.
Kimahesabu hapa utaona kwamba Simba ndiyo inaathirika zaidi na hii inatokana na ukweli kwamba wakati Azam FC inaingia “mzigoni”, imeikuta Simba ikiwa dhaifu mfululizo, viongozi wake na wanachama wameendelea kulala kwenye migogoro au kuamini viongozi wasiofanya jipya, wakati huo Azam FC ikatumia mwanya huo kujijenga.
Ushindani lazima uwe dhidi ya aliye bora, Azam FC imeikuta Yanga ikiwa bora na ndiyo imekuwa ikishindana nayo. Katika kipindi cha misimu miwili au mitatu, Azam imekuwa bingwa mara moja, nafasi ya pili mara mbili. Yanga imetwa ubingwa mara mbili, nafasi ya pili mara moja. Simba imezikosa zote, miaka yote mitatu!
Simba bado wako usingizini, baada ya msimu wa tatu wakiwa watupu, inaonekana kuwa wanakwenda kuukosa ubingwa kwa mara ya nne tena wakiwa na hofu hata ya nafasi ya pili.
Inawezekana kusema Simba itaukosa ubingwa sasa ni kuwakatisha tamaa, lakini hali halisi inasema hivyo au yawepo mabadiliko.
Kwani hakuna asiyejua uimara wa kikosi cha Simba ambacho kina mwendo wa kusuasua, hakiogopeshi na si hadhi ya kikosi hicho kama kilivyokuwa miaka minne au zaidi iliyopita.
Kila siku zinavyosonga mbele, kama Azam FC dhidi ya Yanga itakuwa mechi maarufu. Miaka inahesabika, nayo itaingia katika historia, hata kama ni mwaka 2030, basi inawezekana kuwa ndiyo mechi kubwa kwa kuwa ukubwa wa Simba utaendelea kuwa wa kawaida yenye kikosi cha kawaida kama sasa.
nakubaliana na wewe kuwa na mechi inayovuta wengi kwa sasa, lakini kwa miaka kadhaa sasa ni mechi ambayo inatawaliwa na vurugu sana. Kwa hilo la vurugu tu kwa kweli inapita ukubwa wa mechi za Yanga vs Simba. Binafsi siwezi kuzisifia mechi za aina hii hata kama zinavuta watu wengi zaidi. Leo refa kapigwa, kesho rafu kibao, wachezaji kukunjana, kadi nyekundu za kijinga. Hata mechi ya juzi, Donald Ngoma alikuwa na bahati tu ya kutokupata kadi nyekundu.
ReplyDeleteShikamooooo mzee!
Deleteukubwa wa mechi haungaliwi kwa ngumi uwanjani ata siku moja na ndo mana mpaka msimu uliopita game ya man unite na liverpool ndo game iliotazamwa na watu wengi zaidi duniani kupita el classico,ukubwa wa mechi inatokana na historia,historia ya simba na yanga utaifanya kuendelea kuwa game kubwa mpaka mwisho..az
ReplyDelete