January 15, 2016


Na Saleh Ally
INGEKUWA ‘machozi’ yanalipiwa, basi nisingeweza tena kulipia kwa kuwa nimelia sana kuhusiana na suala la kujengwa kwa viwanja vya wazi ambavyo huwa ni kwa ajili ya wananchi.

Mfano watoto au vijana ambao wanatakiwa kuwa na sehemu za kucheza. Kawaida mipango mji inapokuwa inapangwa, kumekuwa na sehemu za wazi kwa ajili ya wananchi.

Kadiri siku zinavyosonga mbele, zimekuwa zikiuzwa na wahusika wakuu ni waliopewa dhamana au watu wa serikali. Kila mmoja anajua, bila ya watu wa serikali huwezi kuwa na jeuri ya kuangusha mjengo wa nguvu kwenye maeneo ya wazi.

Wakati nakua katika mitaa ya Mji wa Shinyanga na Jiji la Mwanza, tulikuwa tukicheza barabarani kwa kuwa hakukuwa na mipango miji bora ambayo iliacha sehemu za wazi kwa ajili ya watoto. Mara kadhaa, mipira yetu ilikanyagwa na kupasuliwa na magari.

Serikali inalijua hilo, ninaamini nimesema sana, nimekumbusha mara nyingi na upande wa Kitongoji cha Sinza ni mfano ulio wazi. Maeneo mengi ya wazi yamejengwa na wale wenye fedha zao. Serikali inalijua hilo.

Siku chache zilizopita wakati wa hafla ya kumuaga Mbwana Samatta, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi, aliwataka waandishi kwenda kuchimbua na kuandika kuhusiana na alikoanzia Samatta. Wakati anasema hivyo, tayari Championi lilikuwa limeandika kuhusiana na kila kitu siku inayofuata.

Nilipaza sauti na kumueleza Lukuvi kuhusiana na uwanja waliokuwa wakicheza Samatta na wenzake umejengwa kiwanda cha kutengeneza rasta, zile ambazo huwafanya dada na mama zetu kuongeza urembo kwa mwonekano.

Mmoja wa vijana waliocheza na Samatta enzi hizo, Oscar Mmakonde naye alinidokeza kwamba baada ya uwanja huo ulio Mbagala nyuma ya Shule ya St Mary’s kujengwa kiwanda cha rasta, wao walisambaratika na wengine wakaacha mpira.

Alinieleza walianza kucheza kuanzia mwaka 1990, lakini mwaka jana, yaani 2015, kiwanda hicho kikajengwa. Kabla ya hapo waligeuza na kuwa maegesho ya mabasi ya mkoani kwa kampuni moja hivi.

Taarifa za awali zinaeleza hivi, kiwanja hicho ni halali cha mtu. Lakini hakuwa amekijenga siku nyingi, vijana wakawa wanakitumia na wenyeji hasa walikuwa ni Amani FC, pia kulikuwa na timu nyingine mbili tatu.

Kujengwa kwa kiwanda cha rasta, vijana wamesambaratika kabisa. Wengine waliamua kuacha mpira na wengine kama Samatta waliokuwa wameondoka, wameweza kuendelea.

Huenda kiwanja hicho kingekuwa na nafasi ya kutoa vijana wengine. Hata Lukuvi alikubali kwamba Mbagala kuna vipaji. Sasa vipi vinaachwa vinafia Mbagala? Samatta ameshaonyesha hilo, kwangu naona Lukuvi ana kazi ya kufanya katika hili, ili siku nyingine wakati serikali inatoa tuzo basi iwe inajivunia pia ilishiriki.

Serikali ilimpa Samatta fedha na kiwanja cha kujenga nyumba huko Kigamboni, safi sana. Lakini sasa inapaswa kuwapa viwanja vijana ili wakuze vipaji vyao, waviendeleze ili kuzalisha kina Samatta wengine.

Yule mwenye kiwanja aliyejenga kiwanda cha rasta, kama kweli hapo ni kwake, ana haki ya kufanya alichokusudia. Lakini bado serikali inabaki na jukumu la kuhakikisha watoto na vijana wetu wana sehemu maalum kwa ajili ya kucheza.

Miji yote iliyoendelea, ina sehemu za wazi nzuri zinazoendeshwa na kusimamiwa na serikali. Kwetu inashindikana vipi? Wale viongozi wenye tamaa serikalini wamekuwa wakituangusha.

Lakini kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imeamua kwenda tofauti, basi kama inataka mafanikio katika michezo, lazima ikumbuke, vijana hawawezi kuchipukia wakiwa wakubwa, badala yake wanatakiwa kuanza mwanzo na sehemu ya kuanzia ni kwenye viwanja ambavyo vitakuwa huru kwao. Hivyo ilisimamie hilo na Lukuvi, anaweza kuleta mabadiliko kama akiamua.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic