Na Saleh Ally
ALIYEKUWA nahodha wa timu ya soka ya taifa, Nadir Ali Haroub ‘Cannavaro’ ameamua kutangaza kustaafu kuichezea timu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 10.
Cannavaro anaendelea kubaki kuwa nahodha wa mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga pia timu ya taifa ya Zanzibar maarufu kama Zanzibar Heroes.
Cannavaro kama alivyo, hajawa mnafiki kwa kusema sababu ambazo zinaonekana kumkwaza hadi kufikia uamuzi huo wa kutangaza kuitumikia timu ya taifa.
Sababu kuu ambazo alizizungumzia wakati akisema hilo, moja ni lawama lukuki alizorushiwa kwamba amekwisha na alichangia Taifa Stars kufungwa mabao 7-0 na Algeria ikiwa ugenini.
Lakini yeye akaeleza alivyopambana pamoja na wenzake, tena kwa nguvu kuu huku wakiwa pungufu baada ya Mudathir Yahaya kulambwa kadi mbili za njano kisha nyekundu. Ninaamini angekuwa makini, kadi zile zingeepukika.
Sababu ya pili ya Cannavaro ilikuwa ni uamuzi wa kuvuliwa unahodha, akapewa Mbwana Ally Samatta mara tu baada ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora Afrika kwa wanasoka wanaocheza ndani ya Afrika. Cannavaro ameweka wazi, kwamba hapingi yeye kuvuliwa unahodha, wala halazimishwi kubakiwa nao, lakini utaratibu uliotumika kuuchukua kwake kwenda kwa Samatta unaashiria dharau kubwa tena ya kuumiza moyo.
Kwa mara ya kwanza, Cannavaro anasema alijua sasa si nahodha wa Taifa Stars baada ya kuona kwenye runinga, Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa akiwa anatangaza kuhusiana na hilo. Baada ya hapo, kesho yake, kocha huyo akampigia simu kumtaarifu kuhusiana na hilo.
Sasa jaribu kupata picha ya kiungwana, ambayo kamwe haitakiwi kuwa na chembe ya ushabiki. Kwamba wewe ndiye Cannavaro, utasikiaje, utalichukuliaje suala hilo na uamuzi wako utakuwa upi?
Kwanza niwe wazi, niseme naungana na maumivu ya Cannavaro kwamba alichofanyiwa ndiyo mambo ya ‘Kiswahili’ ambayo tumekuwa tukiyapinga na unaanza kupata hisia, kweli kungekuwa na kocha mgeni angeweza kufanya mambo kisiasa na kukurupuka hivyo, ninaamini hapana.
Bado narejea palepale kwamba, kweli kwa miaka yote ya Taifa Stars kwa Cannavaro, alipaswa kuvuliwa unahodha kwenye runinga yeye akiwa hajui lolote? Au Mkwasa alishindwa kufuata taratibu ambazo ni rahisi na laini kabisa, kwa kumtafuta Cannavaro, wazungumze naye, akimalizana naye, azungumze na Samatta baada ya hapo lije suala la kutangaza na ikiwezekana akiwa na wote wawili mbele ya waandishi wa habari.
Sijui, inawezekana kwa kuwa Samatta alikuwa gumzo, kila mmoja akitoa zawadi na pongezi. Mkwasa aliona kumpa ‘unahodha’ ni zawadi. Kama aliona anastahili, basi angefanya hivyo miezi miwili nyuma au baada ya kuipa TP Mazembe ubingwa wa Afrika na ingewezekana kabisa.
Pia angeweza kusubiri hadi kikosi cha Taifa Stars atakapokitangaza, kikiwa kambini, angetangaza hilo na si kukurupuka sasa kwa kufuata tu kwa kuwa upepo unakwenda upande huu.
Uamuzi wa Mkwasa kufanya hivyo akiwa nyumbani kwake, aliona ni rahisi kwa kuwa alimchukulia Cannavaro kama mshikaji, kijana wake, au alimchukulia ‘poa’ tu? Kwangu nasema Mkwasa amevurunda katika hili na anapaswa kujifunza namna ya kuepusha mambo mengine yasiyokuwa na msingi.
Cannavaro alikuwa anajua asingekuwa nahodha milele. Ndiyo maana alihoji kama kweli wengine waliopita kama Shadrack Nsajigwa na wengine, waliondolewa kwa dharau kama yeye? Mkwasa alikuwa mchezaji, kocha wa klabu, kote amepita na anajua machungu ya mchezaji kudharauliwa, sasa vipi kuyajua hayo na kufanya mambo vululuvululu?
Nimetolea mfano kocha wa kigeni, kwamba asingeweza kufanya hivyo, ninaamini hivyo. Mimi ni kati ya wale waliokuwa wakiamini na makocha wazalendo wanapaswa kuthaminiwa na ikiwezekana kulipwa mishahara mizuri na nyumba bora kama ilivyokuwa kwa makocha wageni.
Ninapoona makocha ambao tunawalilia wanaanza kuingia kwenye siasa, kufanya mambo kwa kulipua naanza kuingia woga, najisikia vibaya na kuanza kuona kama tunaowalilia nao si watu makini kwa kuwa wanaweza kutuangusha katika vitu vidogo kabisa ambavyo vilikuwa havihitaji akili nyingi hata kidogo.
Ushauri wangu katika hili; moja, Mkwasa amuite Cannavaro, azungumze naye na kumuomba radhi, hakika amemkosea na hakuna haja ya kupindisha maneno. Kweli Cannavaro kaipigania Stars miaka mingi na anastahili kupewa heshima yake.
Pili; namshauri Cannavaro, kuendelea kuitumikia Stars kila atakapoitwa. Kwangu namuona wala hajazeeka na hapaswi kushinikizwa na mashabiki, wengi wao hawajui mpira na mambo wanayafanya kishabiki. Kocha ndiye ataamua hilo pia ninaamini ana uwezo wa kuitumikia Stars kwa mwaka mmoja, miwili au mitatu ijayo kulingana na anavyojiweka mwenyewe.
Taifa Stars si ya Mkwasa, hata yeye ana haki kama za Cannavaro, hivyo usiwatupe Watanzania wote wanaokuamini na usiachane nao vibaya kwa hili. Dunia ina mitihani, huja, hupita na kwenda. Tafakari.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment