Na Saleh Ally
JANA, Mbwana Samatta aliendelea kueleza alivyokuwa akiishi na mashabiki wa TP Mazembe mjini Lubumbashi na kwingineko nchini DR Congo.
Pia akaelezea ujio wa Thomas Ulimwengu ambaye alijiunga na Mazembe akitokea AFC ya nchini Sweden.
Lakini akasimulia baada ya kipigo cha mabao 7-0 ambacho walikipata Taifa Stars wakiwa nchini Algeria na kusema alichanganyikiwa akawa mara anacheka huku anashangaa. Hajui kipi ni sahihi. Swali la mwisho aliloulizwa lilikuwa kama lifuatavyo.
SALEHJEMBE:Hukujielewa, kuna chochote ulifanya ambacho si cha kawaida?
Samatta: Hapana, niliamua kumuita Uli, nikamuambia aisee hawa jamaa ndiyo profesheno kweli.
Samatta: Nilimwambia Algeria ndiyo profesheno kwa kuwa waliweza kubadili akili zao mara moja tu. Baada ya sare ya mabao 2-2 Dar, wenyewe walibadilika kabisa na ndiyo maana ya profesheno.
SALEHJEMBE:Unafikiri walibadilika wapi hadi kuwa na ubora mkubwa vile tofauti na Dar?
Samatta: Baada ya sare wakaona hatukuwa timu rahisi. Waliporudi kwao, walijua sasa wanakutana na timu bora, huenda walitupandisha katika kiwango cha Misri, Nigeria, Cameroon na nyingine kubwa. Lakini sisi tulikwenda na mawazo tofauti, tukiamini Algeria ni rahisi na wanafungika. Mambo yalikuwa tofauti na walituzidi kweli.
SALEHJEMBE:Unafikiri nini sasa kitaisaidia Tanzania kuondoka katika kitanzi, maana imekwama?
Samatta: Kwa mtazamano wangu siamini kama kutakuwa na kupiga hatua kama wachezaji wataendelea kubaki hapa nyumbani. Wachezaji wajitume watoke waende wakacheze nje ya nyumbani. Angalia pale Afrika Kusini, inawezekana kabisa, watu waende, wajiamini na wajue wakienda nje watajifunza na kuwa tofauti.
SALEHJEMBE: Huenda wachezaji wanataka kwenda, klabu pia zimekuwa zikiwabania?
Samatta: Kwa upande wa wachezaji wajiamini wawe na nia ya kutoka. Lakini viongozi wawaachie wachezaji waende, waache zile tamaa za kutoa madau makubwa kwa wachezaji kutoka Tanzania. Sisi ndiyo tunatakiwa kubembeleza kupata nafasi ili tujitangaze zaidi. Klabu zikiendelea kuwabania wachezaji basi TFF iingilie na kuwasaidia.
SALEHJEMBE: Unafikiri profesheno wengi ndiyo msaada hasa kwa Tanzania kuinuka?
Samatta: Ni sehemu kubwa, kucheza nje unajifunza mengi sana na unapevuka kiushindani. Inakusaidia kama mchezaji, pia unaweza ukawasaidia wenzako kwa kuwa inakuwa ni kama sehemu ya changamoto kutokana na yale unayojifunza unapokuwa ugenini. Niseme yanakusaidia kukua haraka.
SALEHJEMBE:Mchezo wa soka umebadili maisha yako kwa kiasi gani?
Samatta: Nimshukuru Mungu sana, hakika soka imebadili maisha yangu kwa kiasi kikubwa, niseme Napata karibu kila ninachohitaji kwa wakati. Niwe mkweli, Mazembe wanajitahidi kulipa vizuri. Naamini naweza kufanikiwa zaidi nikiendelea kufanya vema.
SALEHJEMBE: Mchezaji kutoka Tanzania, unaendesha Range Rover, nafikiri ni wewe na Ulimwengu tu, unafikiri malipo ndani ya TP Mazembe yanatosheleza au ilikuwa ni mapenzi tu ukalazimika kufanya hivyo ili kuridhisha nafsi?
Samatta: Ukiwa mchezaji wa Mazembe, baada ya msimu mmoja tu, ninaamini utanunua gari unayotaka. Jamaa wanalipa vizuri kwa maana ya mshahara pamoja na posho za mambo mengine.
SALEHJEMBE: Kuna siku niliona umeweka picha ya gari lako mtandaoni, ukaandika maneno ya kuhamasisha, nini ulilenga?
Samatta: Lengo lilikuwa kuwaonyesha vijana mengi yanawezekana, mimi nilikuwa nikipanda daladala kama wao, lakini juhudi bila kuchoka pamoja na maarifa zimebadili mambo.
SALEHJEMBE:Ulisema Mazembe wanalipa vizuri, kama kiasi gani hivi?
Samatta: Kila mchezaji anakuwa analipwa kutokana na makubaliano yake na klabu na amekwendaje pale.
SALEHJEMBE: Unafikiri kuwa mchezaji nje ya nchi kunamsaidia mchezaji kulipwa vizuri?
Samatta: Kwanza uwe unafanya vizuri, lakini ukiwa nje pia unathaminiwa zaidi. Hata hapa nyumbani wachezaji wa nje wanalipwa zaidi, wachezaji watoke nje waende wakapambane. Kule watalipwa zaidi wakifanya vizuri.
SALEHJEMBE: Sasa umeamua kwenda Ulaya, umeshaonana na uongozi wa Genk na mmekubaliana. Mshahara wako au maslahi yako yatazidi kwa kiasi gani yale ya TP Mazembe?
Samatta:……..
USIKOSE SEHEMU YA MWISHO KESHOKUTWA JUMATATU.
0 COMMENTS:
Post a Comment