Serikali imetoa zawadi ya kiwanja kwa mshambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Samatta.
Waziri wa Nyumba na Makazi, William Lukuvi amemkabidhi Samatta hati ya kiwanja hicho kilicho Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa kumpa mkono.
“Hiki ndiyo hati, kukupa mkono tu hivi ndiyo hati yenyewe. Ila ukiwa tayari karibu ofisini kwangu ili nikukabidhi hadi na vijana wakakuonyeshe kiwanja.
Kitakuwa ni kiwanja katika sehemu nzuri kabisa, si zile sehemu watu wamefanya eneo liwe skwata,” alisema Lukuvi.
Pamoja na kiwanja, Lukuvi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumuaga Samatta kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitia fedha taslimu kwa Samatta ambazo hata hivyo hazikuelezwa ni kiasi gani.
“Nimekupa hizi, huu mzigo ni wako kwa niaba ya serikali. Wewe mwenyewe ukiamua kuzionyesha, basi fanya hivyo,” alisema.
Baadaye Samatta alimkabidhi jezi yake TP Mazembe Lukuvi ambaye alisema ataiwasilisha kwa waziri mkuu ambaye alimuwakilisha.
Baadaye Samatta pia alitoa jezi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye amekuwa karibu yake kwa kipindi kirefu kabla hajaenda Nigeria alikoshinda tuzo ya mwanasoka bora na baada ya kurejea.
0 COMMENTS:
Post a Comment