January 8, 2016



Na Saleh Ally
NI siku 54 za maisha magumu kwa Kocha Zinedine Yazid Zidane ‘Zizzou’ akiwa na kazi yake mpya ya Kocha Mkuu wa Real Madrid.

Unakumbuka, Zidane amekuwa na heshima kubwa ndani ya kikosi cha Real Madrid kama kiungo mkongwe na aliyefanya makubwa ndani ya kikosi hicho wakati akikichezea tangu mwaka 2001 hadi 2006.

Baadaye akawa kocha wa vijana, kocha msaidizi chini ya Carlo Ancelotti, sasa ndiye bosi mkuu baada ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa kocha mkuu, Rafa Benitez.

Maswali yamekuwa mengi sana kama kweli gwiji huyo atauweza mziki wa Real Madrid akiwa katika nafasi ya kocha kwa kuwa inawezekana ndiyo kiti cha moto au matatizo zaidi kwa makocha duniani kote.



Hofu ya wengi, Zidane atapoteza ile ladha ya heshima ya gwiji, kwani kiuwezo kama kocha hana rekodi za kufanya vizuri na klabu yoyote hata ya ligi kama Ufaransa, Ureno au Ubelgiji. Sasa vipi Real Madrid?

Pia Madrid wanapofikia wanaona wanayumba, hawajali mbele yao ni nani au kawafanyia nini. Maana hata Benitez ni mtu wa Madrid, ameibukia hapo na anajulikana kama mtoto wa Madrid, lakini kabla ya miezi saba, wamemfungashia virago.

Kawaida ya Madrid huchukua makocha bora kabisa, vipi safari hii wamekwenda na ule mfumo wa Barcelona kuchukua wachezaji wao wakongwe pale nyumbani? Watauweza mfumo huo? Hata kama walikuwa wanampika Zidane, kweli “amekwiva?”

Wakati maswali mengi yanaendelea, Zidane atakuwa na kazi kubwa ya kuyajibu katika siku hizo 54 kuanzia Januari 9, yaani kesho hadi Machi 2.

Ndani ya siku hizo atakuwa ana mechi 10 za kuiongoza Real Madrid. Tisa kati yake ni za La Liga na moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.



Katika mechi hizo 10, mechi tano zitakuwa nyumbani na tano ugenini. Kazi kubwa kwa Zizzou ni kutafuta pointi 27 za La Liga huku akiwa anataka kuifunga Roma katika Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 Bora akiwa ugenini mjini Roma Italia.
Maswali mengi ya kama kweli ana uwezo au ataiweza kazi hiyo ya “kiti moto” ambayo imewashinda makocha magwiji kabla ya kupewa yeye kocha “kinda”, yatakuwa yakipatikana taratibu kadiri siku zinavyosonga mbele.

Hata hivyo, Zidane analazimika kufanya kazi kubwa ya ziada kuhakikisha anakiunganisha kikosi hicho kwa maana ya kuwa pamoja na wenye furaha.
Uwezo mkubwa wa wachezaji wengi wa Madrid unahitaji furaha na amani ya moyo ili kuwafanya wawe tayari kupambana na hiyo, maana yake ni suala la kisaikolojia zaidi ambalo anatakiwa kucheza nalo.

Kingine ambacho kinaweza kumsaidia Zidane ni kuwa karibu au angalau kwa muda kuizidi nguvu ya “Mafaza” wa kikosi hicho kama Sergio Ramos, Pepe na Cristiano Ronaldo ambao wamekuwa tatizo kwa makocha kadhaa ambao walionekana kutoenda nao sawa.



Zidane ameichukua Madrid akiwa bado na ile heshima yake ya ugwiji. Hivyo ana nafasi ya kuheshimika au kukubalika kwa kuwa pia wengi walipenda kuwa kama alivyo yeye au alipofikia.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa, huenda ni kati ya makocha wadogo kabisa na wasio na sifa yoyote kati ya waliowahi kupewa kazi ya kukinoa kikosi cha Madrid na anaweza kuleta mabadiliko na kuwafanya watu waamini kumbe hata makocha wasio magwiji, wanaweza kuibadili Madrid. Lakini hii ni kama tu atafanikiwa, akifeli ataifanya Madrid milele ibaki na mtindo uleule, kocha bora zaidi ndiye mwenye nafasi ya kuinoa, akiharibu, hata miezi miwili, aende zake.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic