Bondia Mtanzania, Francis Cheka ameibuka na ushindi kwa kumpiga Geard Ajetovic kwa ushindi wa pointi huku majaji wote wakimpa ushindi. Sasa ndiye bingwa mpya wa mabara, ubingwa ambao aliupoteza kwa kupigwa nchini Russia mwaka 2014.
Ajetovic raia wa Serbia anayeishi nchini Uingereza alipinga baada ya kudai ndiye alicheza vizuri zaidi.
Katika pambano hilo kuwania ubingwa wa Mabara, Cheka alionekana kupiga ngumi nyingi za kudokoa lakini hazikuwa na nguvu sana kama za mpinzani wake aliyepiga ngumi chache lakini kali.
Mashabiki wengi waliokuwa kwenye Viwanja vya Leaders walionekana kuwa na hofu kutokana na Ajetovic kuachia ngumi kali za kushitukiza ingawa Cheka alipiga nyingi zaidi za kudokoa zilizomsaidia kupata pointi nyingi.
Hata hivyo, inawezekana ngumi nyingi za kudokoa ndiyo zilizompa ubingwa huo Cheka dhidi ya Ajetovic ambaye alionekana hatari kwake tokea mwanzo.
Cheka alishindwa kuonyesha cheche tokea mwanzo mwa mchezo huo baada ya kupingwa hadi kudondoka.
Lakini kadiri mchezo unavyosonga mbele, angalau akaanza kuonyesha cheche na kubadilika ingawa mpinzani wake aliendelea kupiga ngumi kali.
Raundi ya tisa, Cheka alichanika na kuanza kuvuja damu, lakini bado alionekana kuwa mvumilivu na kuendelea kupambana akiwa amepania kulipa kisasi.
Kilichoshangaza, raundi za mwanzo Cheka ambaye aliwahi kupoteza pambano nchini Uingereza dhidi ya Ajetovic, alionekana kama muoga fulani hivi.
Cheka alionekana mwoga, huenda kutokana na umakini aliotaka kuuhakikisha kwa kuwa anajua ukali wa ngumi za Ajetovic ambaye hata hivyo, mwishoni alionekana kuchoka.
0 COMMENTS:
Post a Comment