February 10, 2016



Kiungo mkongwe wa Simba, Mwinyi Kazimoto anatuhumiwa kumpiga mwandishi wa habari, hali iliyosababisha afikishwe katika kituo kikuu cha Polisi cha Shinyanga.

Kazimoto amefikishwa katika kituo hicho kilicho karibu kabisa na hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa madai ya kumshambulia mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti, Mwanahiba Richard.

Imeelezwa, Kazimoto alimshambulia Mwanahiba baada ya mazoezi ya Simba yaliyofanyika katika Uwanja wa Kambarage ulio katika eneo la Majengo mjini Shinyanga, leo.

Mara baada ya mazoezi, inadaiwa Kazimoto aliyechipukia kisoka mkoani Mwanza, alimvamia alimvamia Mwanahiba na kumpiga akidai aliandika stori kwamba kiwango chake pamoja na wachezaji wengine katika mechi mbili za Mbeya City, pia Prisons ya Mbeya hakikuwa kizuri na wanapaswa kuchunguzwa.


Kazimoto alionekana kutofurahishwa na habari hiyo iliyoonekana ni kama tuhuma, hivyo kupandwa na hasira hadi kuingia katika mgogoro huo na Mwanahiba.

Inadaiwa baada ya kipigo hicho, Mwanahiba aliriripoti katika kituo hicho cha polisi na kupewa hati mashitaka (RB) yenye yenye namba SHY/RB/895/2016, fomu ya matibabu (PF3) kisha akapelekwa hospitali kwa matibabu.


Kazimoto hakupatikana kulizungumzia suala hilo, pia hakuna kiongozi wa Simba aliyelizungumzia, huku kukiwa na hekaheka ya kutaka kulimaliza kwa amani jambo ambalo linaonekana kupingwa na upande wa wanaolalamika.

MWANAHIBA RICHARD

Kwa upande wake Mwanahiba, alisema aliandika stori iliyokuwa ikieleza viongozi wa Simba kutoridhishwa na baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo Kazimoto baada ya wao kupoteza mchezo kwa kufungwa na Prisons  kwa bao 1-0 mjini Mbeya katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

"Ilikuwa ni stori ya mwaka jana, leo Kazimoto akaniita na kuanza kuniuliza akitaka nimwambie kiongozi gani aliyeniambia. Nikamueleza si kazi yake, kifupi niliandika na anajua kama hilo lilitokea.

"Alipoona nimemzidi hoja, akaanza kunidhambulia kwa ngumi na mateke. Akanipiga hadi aliponiumiza kichwani, wakati huo wenzake walikuwa kwenye basi wanashuhudia, ndiyo Mgosi akawahi kushuka na kuniokoa," alisema Mwanahiba.

Lakini Mhariri wa Mwanaspoti, Michael Momburi amesema suala hilo linashughulikiwa.

"Kweli hilo suala lipo, limefikishwa polisi na sisi tunaendelea kufuatilia. Hakika si suala sahihi na halifurahishi na tayari tumelikabidhi suala hilo kwa mwanasheria wa kampuni analishughulikia kwa kushirikiana na RPC wa Shinyanga," alisema Momburi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic