February 3, 2016


Na Saleh Ally
NINAAMINI haitakuwa vibaya kama nitaanza kwa kutumia methali mbili za Kiswahili ambazo zinaweza kunirahisishia njia ninayotaka kupita kwa ajili ya kuwaeleza jambo husika.

Tuanze na ule unaosema, “Jaribu huleta dhahabu na matulubu”, huu unamaanisha unapojaribu jambo, mambo mawili yanaweza kutokea; kufanikiwa au kufeli, hivyo lazima uwe tayari kukubali.

Methali nyingine inasema hivi; “Jaribu huleta fanaka”. Kwamba unapojaribu jambo fulani, inawezekana kupata manufaa ambayo ndiyo fanaka. Mimi nikaamua kulifikisha ninaloliamini, Simba wakikubali wanaweza kufanya hiyo jaribu ikiwezekana wapate fanaka.


Ukiangalia kikosi cha Simba, kwa sasa kimeanza kuimarika. Inawezekana kabisa viongozi wapo karibu, wapo tayari kusaidia na wanaonyesha kwamba wanafurahishwa na mwendo wa kikosi chao, hilo ni jambo zuri kwa wakati husika.

Wakati wanakwenda mbele, katika mechi takriban tatu tangu beki wake wa pembeni Hassan Ramadhani ‘Kessy’ arejee kazini, ameonyesha vitu vingi sana tofauti ukilinganisha na awali.
Achana na kwamba ameweza kufunga bao moja ndani ya mechi mbili. Lakini Kessy ameonyesha uwezo mkubwa sana.

Ameonyesha uwezo mkubwa katika mambo kadhaa, ninaamini kama Kocha Jackson Mayanja atajiamini na kumpanga kama kiungo mshambuliaji au winga, basi Simba itakuwa imepata Emmanuel Okwi mpya baada ya mwaka mmoja ujao.
Kulinganishwa na Okwi si jambo dogo, mchezaji anatakiwa kufanya kazi ya ziada. Lakini kama unakumbuka, baada ya kutua Simba akitokea SC Villa, Okwi alilazimika kupambana na kufanya kazi kwa juhudi kwa zaidi ya msimu mmoja ili kuanza kuonyesha uwezo wake ambao umeacha gumzo Msimbazi.

Kessy anaweza kuwa Okwi, ni suala la muda na kuaminiwa tu. Inawezekana hivyo kwa kuwa kuna vitu ameonyesha ambavyo wachezaji wengi hawana na akiendelea kupambana bila ya kuvimba kichwa au kukubali kukatishwa tamaa, basi atakuwa hashikiki.


Kasi:
Kessy ana kasi ya juu kabisa ambayo inaweza kumsaidia kuwa hatari kila timu yake inaposhambulia. Hii utaiunganisha na kasi yake ambayo imekuwa ikimsaidia kupanda haraka na pia kurejea kwa kasi ya juu kwenda kulinda tena.
Kama atakuwa anacheza kama winga au kiungo wa ushambuliaji, nguvu nyingi ataitumia upande wa zone ya wapinzani na kasi yake itaongezeka kwa kuwa atacheza si katika eneo kubwa zaidi kama anapokuwa mlinzi.

Krosi:
Inajulikana, Kessy ni mzuri katika kupiga krosi, ukimuweka kwenye wachezaji watano wanaopiga krosi nzuri zaidi Tanzania Bara, hautakuwa umekosea.
Ana uwezo wa kupiga krosi nzuri akiwa katika mwendo kasi lakini mara nyingi anajua ifike sehemu gani. Unamkumbuka Okwi katika kazi hii? Kweli alikuwa ni ‘Master’.

Kujiamini:
Hali ya kujiamini imepanda kwa kiasi kikubwa hasa baada ya kurejea uwanjani. Kessy wa leo si Kessy wa jana, ndiyo maana ana uwezo wa kupiga chenga au kukokota mpira mbele ya mabeki wengi akiwa analenga anachotaka kufanya.

KESSY

Amefanya hivyo zaidi ya mara sita katika mechi mbili. Lakini ameweza kufunga bao safi akiwakokota mabeki, akatoa mpira, akapewa na kufunga vizuri kabisa. Haya yalikuwa mambo ya Okwi.

Umaliziaji:
Tunajua, mabeki wengi ni wagumu katika ufundi wa umaliziaji. Lakini bao la Kessy dhidi ya African Sports lilikuwa ni sehemu ya mwanga, kwamba “huyu bwana mdogo” amebadilika kabisa.
Alimalizia kama mshambuliaji bora au hatari anayecheza nje ya Tanzania. Hii ni nadra sana kwa hata washambuliaji, hii ni silaha nyingine aliyokuwa nayo Okwi.

UGANDO, KESSY NA KIIZA WAKISHANGILIA BAADA YA BAO ALILOFUNGA KESSY

Kwa kifupi kumfikia Okwi kunahitaji kazi kubwa, lakini Kessy anaonyesha hata asipokuwa kama Okwi kwa maana ya umahiri, inawezekana akafanya vizuri au vizuri zaidi.

Kikubwa ni kwake kutoanza kubadilika kwa mafanikio kidogo. Lakini pia kwa uongozi wa Simba na benchi la ufundi kuonyesha linathamini kazi yake kama sehemu ya kumpa morali.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic