Ile kesi ya wasemaji wa klabu kongwe hapa nchini, Haji Manara wa Simba na Jerry Muro wa Yanga, imefika mbali baada ya kutua mikononi mwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.
Manara anamshutumu Muro kutokana na kauli zake za kejeli anazozielekeza kwake na Klabu ya Simba kwa jumla huku akienda mbali zaidi na kusema amepanga kumpeleka polisi.
Manara licha ya kumtuhumu Muro, pia analilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kukaa kwao kimya bila ya kumchukulia hatua Muro kutokana na kauli zake hizo za kejeli anazozielekeza kwao.
“Nimeongea na Waziri Nape na amesema atalishughulikia suala hili na kumaliza tofauti zetu katika suala zima la kulifanya soka letu kutokuwa na migogoro, hivyo tumekubali na hivi karibuni atakutana nasi kulimaliza jambo hilo,” alisema Manara.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, amesema: “Masuala yote ya kinidhamu yapo katika Kamati ya Nidhamu ya TFF ambapo Machi, mwaka huu wahusika wa kamati hiyo watakaa kujadili hayo yote na kuyatolea ufafanuzi.
“Msione yanachelewa mkadhani TFF inafanya makusudi, bali wahusika hawapo karibu na mpaka kukutana kwao inachukua muda mrefu, ndiyo maana hali hiyo inatokea.”
0 COMMENTS:
Post a Comment