March 9, 2016


Beki wa kati wa Azam FC, Said Moradi amesema anaelekea kumaliza mkataba wake na timu hiyo na yupo tayari kujiunga na timu yoyote ya Ligi Kuu Bara lakini chaguo lake la kwanza ni Simba au Yanga.

Mkataba wa mwaka mmoja wa Moradi na Azam unamalizika Mei 30, mwaka huu na hadi sasa hajaambiwa lolote kuhusu mkataba mpya hivyo ameanza kujiweka sokoni ili asikose timu msimu ujao wa ligi kuu.

Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo amesema jana Jumanne kwamba, mkataba wa mchezaji huyo unaelekea ukingoni  bila ya kuambiwa lolote na uongozi wa Azam na hivyo anaona bora asepe zake.

“Mkataba wake na Azam unaisha Mei 30, mwaka huu, hajaambiwa lolote hadi sasa ndiyo maana anasema yupo tayari kwenda popote penye maslahi, hata iwe Simba au Yanga.

“Amesema atafurahi zaidi akienda Yanga kuongeza ulinzi wa kati na Yondani (Kelvin) ila itategemea zaidi na atakachoambiwa na Azam maana ndiyo timu yake ya sasa,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Moradi ambaye alisema kuwa ni kweli mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu na yupo tayari kwenda popote.

“Mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu, nipo tayari mimi kwenda popote lakini lazima iwe timu kubwa kama Simba au Yanga, lakini kwa sasa mimi bado ni mali ya Azam na wakizungumza nami nitawapa kipaumbele,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Ashanti United, Simba na Kagera Sugar.

Katika kikosi cha Azam, Moradi amekuwa akicheza beki ya kati sambamba na Pascal Wawa na David Mwantika katika mfumo wa 3-5-2 ambao huchezwa na mabeki watatu wa kati.

Wikiendi iliyopita alishirikiana vyema na wenzake kuwazuia washambuliaji wa Yanga wakiwemo Amissi Tambwe na Donald Ngoma na kulazimisha sare ya mabao 2-2.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic