March 11, 2016



Na Saleh Ally
KAWAIDA linakuwa jambo jema yule anayeitwa mkongwe akawa mfano wa kuigwa kwa wale anaowaongoza au vijana wake. Hii inaweza kuwa katika maisha ya kawaida au jambo fulani.

Kama ingekuwa ni kazini, kijana aliyetokea shuleni, angependa kujifunza namna ya utendaji bora kutoka kwa mzoefu aliyemkuta kazini. Baada ya hapo pia anaweza kujumlisha ubora wake kikazi na kufanya kitu bora zaidi.

Kijana huyo kutoka shule, anaweza pia kufanya jambo, mkongwe au mzoefu kazini pia akajifunza. Lakini itakuwa ni kichekesho kama kijana aliyetokea shule ndiye atakuwa anatoa mambo ya kujifunza kwa yule mkongwe kila kukicha pale kazini.

Ninaita kichekesho kwa kuwa mzoefu tayari anajua ubora na changamoto za kazini. Mimi leo nimeamua kuzungumzia mwendelezo wa kichekesho kutokana na wakongwe kazini, yaani Yanga na Simba kuendelea kujifunza kila kukicha kupitia kijana kutoka shule, ninamaanisha Azam FC.


Yanga imeanzishwa mwaka 1935, Simba ikazaliwa mwaka 1936. Azam FC imezaliwa 2004 lakini wakongwe hao wamekuwa wakisubiri kujifunza kupitia kijana huyo huku wao wakiwa hawana lolote ambalo ni jipya ambalo kijana Azam anaweza kujifunza kwao.

Azam FC, wameondoka nchini juzi wakiwa ndani ya suti safi kabisa kikosi kizima. Walionekana katika picha kama ambavyo unaweza kuwaona Manchester United, Real Madrid, Chelsea, Arsenal na timu nyingine za Ulaya zinapokuwa safarini.

Baada ya picha za wachezaji wa Azam FC kusambaa mitandaoni. Baadhi ya mashabiki walianza kuponda ikiwa ni pamoja na kusema vipi wavae suti huku wakiwa wamebeba mabegi ya mgongoni.

Katika hali ya kawaida, unaona ni mashabiki wanaokerwa na maendelea ya upande mwingine. Wakati walitakiwa kuwapongeza na kuona ni jambo jema ambalo linaweza kuigwa.


Uwanja binafsi wa timu ambao unatumika hadi sasa wanao Azam FC, wao wameagiza jezi zao wenyewe ambazo zinajulikana kama mali ya Azam FC. Timu hiyo ina akademi bora kabisa ya vijana kuliko Yanga na Simba. Wana eneo lao maalum kwa ajili ya mazoezi. Usisahau wanamiliki zaidi ya viwanja viwili vya mazoezi, hosteli, bwawa la kuogelea, gym ya uhakika na kadhalika.

Vitu vyote hivyo, wakongwe kazini Yanga na Simba, hawana kabisa. Ikiwa wanavyo basi vitakuwa vimejaa kasoro kwa maana ya hivi; vibovu, havitumiki au havijajengwa lakini wao ndiyo wenye maneno mengi.

Kama tunazungumzia maendeleo au mafanikio, hatuna budi kuona kwa wenzetu hasa barani Ulaya ambao wana mafanikio makubwa kisoka wao hufanya hivyo kwa wachezaji wao kuvaa mavazi yenye mwenekano wa kuvutia na heshima hasa.


Mara ya mwisho, Taifa Stars walivaa suti wakati timu ilipokwenda Ivory Coast kushiriki michuano ya Chan. Leo Azam FC wamevaa wakienda kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest nchini Afrika Kusini.

Maendeleo ya soka yana vitu vingi. Yanga na Simba bado zina nafasi kubwa ya kubadilika na kuachana na kuendesha mambo kienyeji kama zilivyokuwa zimezoea.
Mnaweza kudharau, lakini kuvaa suti ndiyo sehemu ya mabadiliko na kupiga hatua kwenye jambo moja kwenda jingine.
Huenda wako watakaokuwa wanaona kama mzaha. Azam FC inakwenda inabadilika jambo moja hadi jingine. Itafikia siku Yanga na Simba wanashituka, iko mbali sana na kuikamata itakuwa ni hadithi isiyokuwa na stelingi.


Suti inaweza isiwe pekee lakini Azam FC imepiga hatua ya vitu vingi wakati Yanga na Simba zikiwa zimelalia kigezo cha ukongwe na wingi wa mashabiki. Zikumbuke kila kukicha, kuna kizazi kipya ambacho hakika kitapenda wanaofanya mambo kwa mtazamo unaoendana na wakati wao.

3 COMMENTS:

  1. Saleh mpira sio mavazi kama ingekuwa mavazi ndio kusakata kabumbu basi korea kusini ingekuwa bingwa kombe la dunia 2014 kule Brazil.Angalia hata England wanavyovaa suti nzuri za bei mbaya wakati mpira hakuna!

    ReplyDelete
  2. Hapo bwana saleh umechemka, simba ndio timu ya kwanza kuvaa suti kumbuka bwana, Alhaji Ismail Aden Rage Rais aliyepita anawapa vijana suti wanakwenda kucheza na Algeria hata shaffih anajua sijui wewe ulikuwa wapi.
    tuomba radhi wanamsimbazi tafadhali.

    ReplyDelete
  3. Ndio maana napata shida kuwaelewa waandishi wa bongo!! vitu vingine sio hata vya kuandikia makala. Kuvaa suti kwanza lazima ujue inaendana na hali ya hewa, sijawahi kuona timu yoyote including brazil walivyokuja bongo kuja wakiwa wamevaa suti. Hata barca juzi wakati wanaenda emirates kuwavaa arsenal walikuwa casual tu. Hata kama mnawependa sana Azam, basi angalieni mambo ya msingi ya kuandika na sio kusifia hata vitu ambavyo havina tija!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic