LIGI kuu Bara na Ligi nyingine kubwakubwa zile duniani zote kwa sasa zimesimama kupisha maambukizi zaidi ya Virusi vya Corona ambavyo vinaitikisa dunia kwa sasa.
Hapo bado tunapaswa tukumbushane kwamba Virusi vipo na tahadhari ni muhimu kuifuata sio jambo la kuchukulia utani na kudhani halituhusu sisi kisa tupo Afrika.
Wote tunahusika kwani tupo kwenye hii sayari ya tatu ambayo ni dunia ambayo ina mambo mengi yanayotokea kila iitwapo leo.
Hakuna kitu kama hicho tunaona tayari mpaka kwenye bara letu Virusi vinapoteza nguvu kazi pamoja na kusimamisha shughuli nyingi za muhimu kwa ajili ya maendeleo yetu.
Kitu cha msingi bado ninasisitiza katika hili tusiache kuomba dua njema kwa Mungu ili tupite salama katika mapito haya ambayo ni magumu.
Wengi ambao wamekuwa wakipuuzia ule utaratibu unaowekwa na Serikali pamoja na wataalamu wa afya tunaishi nao hivyo tusisahau kuwakumbusha umuhimu wa kuzifuata bila shuruti.
Tusisahau pia kusema asante kwa Mungu kwa kuzidi kutulinda na kutupa afya ya kukutana tena wakati huu na tunaona licha ya maambukizi ambayo yapo nchini bado haijafikia ile hali ya kutisha.
Hakika katika hilo pia tusiache kusema asante na kuomba pia kwa ajili ya wengine walio nje ya Tanzania wawe salama kwani tukisema tusiwajali tunajiangamiza wenyewe.
Fikiria nchi ya Misri kuna watanzania wengi ambao wanaishi huko pia hata nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania Himid Mao yupo huko hivyo tusiwasahau hawa ndugu zetu pia.
Wakati huu napenda kuziambia timu kwamba ikiwa ni muda wa siku 30 unakaribia kumeguka ni jukumu lao kutazama sasa namna gani wanaweza kurejea tena kwenye ushindani iwapo mambo yatakuwa shwari.
Viongozi wanatakiwa kupitia mipango kazi yao ambayo walikuwa wamejiwekea ili kuona ni kwa namna gani wameweza kufanikiwa kuyafikia malengo yao.
Wale ambao hawakufanya jambo lolote bado wana muda kidogo uliobaki kuanza kujipanga upya kwani hekaheka zikianza hakuna ambaye atakuwa na nafasi ya kujipanga tena.
Uzuri ni kwamba mchezo wa mpira haufichiki kila mmoja anaona na anatambua kwamba hawa walikuwa seriazi ama walikuwa wanadanganya kwa kudai kwamba wametoa program kwa wachezaji kumbe hamna kitu.
Wachezaji muda wenu unazidi kwenda mbele pia itakuwa ni fursa kwenu kuendelea kujijenga zaidi na kulinda vipaji vyenu.
Kila kitu kinawezekana kurejea kwenye hali yake ya kawaida iwapo hatutasahau kufuata kanuni hivyo wote katika hili tunapaswa kuwa na lengo moja kwenye mapambano na Corona.
Basi mkiwa nyumbani na mkiwa mnatoka msisahau kwamba dunia inapambana nanyi pia ongezeni juhudi katika kupambana na kuwa balozi kwa wengine kuhusu Corona.
0 COMMENTS:
Post a Comment