March 11, 2016



Na Saleh Ally
MSANII mkongwe nchini wa filamu, Single Mtambalike ‘Rich Richie’ ameibuka mshindi katika katika African Magic People’s Choice Awards, tuzo zilizotolewa Jumamosi iliyopita jijini Lagos, Nigeria.

Richie ameshinda tuzo hiyo ikiwa ni baada ya miaka 18 ya kufanya kazi hiyo bila kupata tuzo. Safari kupitia filamu yake ya Kitendawili, amefanikiwa kuibuka mshindi katika kipengele cha filamu bora ya Kiswahili.

SALEHJEMBE, ilifanikiwa kufanya naye mahojiano jijini Lagos na mambo yalikuwa hivi;

SALEHJEMBE: Kabla ya kutwaa tuzo hii, ulikuwa unaionaje Bongo Movie, unafikiri itasaidia?
Richie:Ninaamini Bongo Movie itarudi kwenye heshima yake. Kuona ni kuamini, wataona mimi nimechukua tuzo, Lulu pia. Lakini wasanii Watanzania zaidi ya wawili walipata nafasi ya kushiriki. Ona sasa na Serikali nayo imejitokeza kuwa karibu nasi, hii itasaidia pia.


SALEHJEMBE: Kwa filamu mnazotengeneza, unafikiri zinaweza kuingia kwenye ushindani wa kimataifa na kushinda hasa?
Richie: Inawezekana, wenzetu wamepiga hatua sana. Lakini hatupaswi kukubali na kukaa, badala yake tupambane hasa kuhakikisha tunafanikiwa. Si kazi rahisi lakini lazima tushirikiane.


SALEHJEMBE: Bongo movie mnaonekana hamjatulia, hamna ushirikiano na majungu ni rundo. Tatizo ni wakongwe hamtaki ushindani, au vijana nao hawana nidhamu kikazi?
Richie: Yote yanawezekana,  tunaweza kuwa sisi au wao. Lakini jambo jema ni kila upande kujipima, tujitazame na kuamsha hisia za umoja na kutaka kila mmoja afanikiwe. Kwa njia nzuri ninaweza kusema ni ushirikiano.


SALEHJEMBE: Ukiangalia Marekani au hata Nigeria, inajulikana hawa wanaigiza filamu za vichekesho, hawa wanaigiza za drama au vinginevyo. Nyumbani Tanzania hamfanyi hivyo, huoni inachangia nyie kufeli?
Richie: Kweli hii nayo inachangia kwa kiasi Fulani. Lakini vizuri mcheshaji achekeshe, anayecheza tamthilia acheze tamthilia. Ukiiangia sehemu nyingine unaweza kuingia kidogo. Angalia kwenye muziki, wanaoimba wanaimba, wanaorap wanafanya hivyo. Lakini wanaweza kushirikiana

SALEHJEMBE: Mnakosa ubunifu, hamjui kuanzisha. Mtu mmoja akicheza filamu ya porini, ikifanya vema wote wanafanya za aina hiyo, huoni majiangusha wenyewe?
Richie: Kweli mtu mtu akicheza filamu ya Uswahilini ikafanya vema, basi kila mtu anataka acheze ya Uswahilini. Kufuata mkumbo kunatuangusha. Lazima watu wakubali kutulia, kutengeneza hadithi bora kabisa ndiyo zitakazozaa filamu bora pia.

SALEHJEMBE: Umeigiza kwa miaka 18 bila ya kupata tuzo, nini ulikuwa msukumo na hukuwahi kukata tamaa?
Richie: Ni mtu niliyetaka kitu Fulani, familia yangu hasa mke wangu hakushoka kuniambia niendelee kupambana. Nashukuru sana kwa hilo.

Championi: Hayo tu yaliyosha kukufanya uendelee bila ya kuchoka?
Richie: Yako mengine kadhaa, mfano kuendelea kujifunza bila ya kuchoka. Sijawahi kuamini ninajua sana. Nimeendelea kujifunza na kufunzwa na wataalamu. Pia malezi yetu kuanzia kipindi cha ‘Mambo Haya”. Tulikuwa tukifundishwa mengi na mafunzo yetu yalikuwa bora. Kama vile utengenezaji was tori, kila wiki tulikuwa tukitengeneza kisa. Hii ilitusaidia kuwa wabunifu katika utunzi na uigizaji. Vijana wa sasa hawafanyi hivyo ingawa wako wanaojitahidi.

SALEHJEMBE: Hakuna kingine zaidi ya hivyo?
Richie: Heshima, kujali na kuithamini kazi yako.

SALEHJEMBE: Haumaini ushirikiano na nguvu moja inaweza kurudisha upendo na imani kwa watazamaji wa filamu?
Richie: Kweli ushirikiano ni muhimu pia nimesema sana. Nakubali kuna sehemu hakuna upendo lakini pia tunahitaji muda wa kutengeneza majina. Halafu baada ya hapo ifuatie kutengeneza fedha.

SALEHJEMBE: Huoni kama umechelewa kupata tuzo kutokana na muda uliofanya kazi?
Richie: Nakubali kabisa nimechelewa sana. Lakini najivunia uwezo wangu wa uvumilivu hadi sasa. Wako wameanza miaka mitano tu wamekata tamaa. Anayeganga njaa ndiye anayekata tamaa. 

SALEHJEMBE: Wakenya wameiangusha sana Tanzania, safari mmewaangusha, unafikiri nini kipya kilichosaidia?
Richie: Tulifeli sana katika utayarishaji wa filamu zetu. Sasa mambo yamebadilika, hii ni changamoto. Lazima tujue walioshindwa wanarejea kwao kujipanga. Waandaaji wakubwa wa Tanzania wasiangalie kuuza sura tu, tupambane kujenga heshima yetu na ya nchi na baadaye tutengeneza fedha.

SALEHJEMBE: Baada ya kifo cha Kanumba, wako waliokata tamaa kabisa kuhusu Bongo Movie. Leo umetwaa tuzo hii, itawasahaulisha Watanzania machungu yao?
Richie: Mimi nikuambie kitu, hata aondoke nani filamu za Tanzania zinahitaji mfumo bora tu na si mtu. Kila mmoja afanye kazi yake bora.

SALEHJEMBE: Marekani wanatakamba, kwenye filamu watu wanatukana, nyie hamfikii huko.Hii inawaathiri?
Richie: Kuna uoga sana, lakini filamu inahitaji uhalisia. Jambazi hawezi kuwateka watu huku akiwalazimisha. Angalau atukane kidogo. Ndiyo maana unaona watu wanajichanganya unaona director kakubali jambazi avue viatu kwenda kuteka watu.

SALEHJEMBE: Sasa ulitaka mtukane ili filamu ziwe bora?
Richie: Ndiyo, jambazi akiingia lazima atukane aseme (tusi), halafu atie mkwara na tena atukane (tusi tena kubwa). Huo ndiyo uhalisia. Jambazi anapoingia na lugha laini haiwezi kuwa halisi. Msichana anakwenda kujiuza, akivaa kimini filamu inafungiwa. 

SALEHJEMBE: Hivyo hata wanaooga waonyeshwe?
Richie: Hapana, kuna vitu vya kuonyesha. Mfano kula denda, tunaona kote na inajulikana. Hapa tunalinda maadili lakini kama tunashindana na soko la dunia. Basi kuwe na vipengele. Kuna filamu ambazo hawatakiwi kuangalia watoto. Hilo hata Marekani wanafanya kama filamu ina lugha chafu au picha ambazo umri hauwaruhusu lakini si kuwabana wasanii tu!




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic