May 23, 2016

KIONGERA

Na Saleh Ally
LIGI Kuu Bara imefikia tamati jana, sasa walio na ubingwa wanaendelea na yao, waliobaki kwenye ligi wanaanza kujipanga upya na waliopanda, pia watakuwa wanajiweka vizuri kuanza na maisha mapya.

Kila la kheri waendako walioteremka daraja, inawezekana kabisa kujipanga na kukaa vizuri, mwisho wakarejea lakini lazima wajipange kweli maana daraja la kwanza kugumu hasa.

Wakati mambo ya ligi kuu yaliyopita yanabaki kama rekodi au historia, sasa ni maandalizi ya msimu ujao lakini ni muhimu kufanya tathmini kwa yaliyopita.

Kwanza kabisa ninaanza na wachezaji wa kigeni waliokuwa wanazitumikia timu mbalimbali nchini. Wapo walioonyesha wanastahili na wengine walikuwa ni watalii na wajaza nafasi ambao wanastahili kurejea kwao mara moja.

Msimu uliopita, timu zilililia kuongezewa wachezaji wa kigeni, huenda Yanga pekee ndiyo ilifaidika kidogo na kiasi cha wachezaji saba wa kigeni lakini zilizobaki zilijaza asilimia kubwa ya wachezaji wenye viwango vinavyolingana na wale wa nyumbani au chini yake.

NIMUBONA
Wapo waliogeuka kuwa waigizaji badala ya wacheza soka ambao wana msaada na wanaopaswa kuwa msaada. Lazima tukubali, hata kama wanasajiliwa na Yanga, Simba, Azam FC, Coastal Union au timu nyingine, bado hizi ni timu za Tanzania, lazima tulinde maslahi yake.

Timu za Tanzania zinaposajili wageni, zinastahili kupata faida kwa kuwa zinawalipa fedha nyingi kuliko wazawa, zinawalipia nyumba na hata posho inakuwa ni ya kutosha. Kama hawafanyi kazi vizuri, wanauza maneno au wanageuka wachonganishi au wanafiki, basi vizuri wakarudi kwao mara moja na kutupa nafasi ya kuendelea kukuza wachezaji vijana.

Yanga:
Hawa walionekana kufaidika baada ya wachezaji wake raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kuonekana kweli ni “majembe” na walikuwa mfano uwanjani. Watu wa kupambana na kamwe usingewasikia wanalaumiwa kwa kuchonganisha kati ya uongozi wa Yanga na wachezaji kwa lolote lile.

Hamisi Tambwe raia wa Burundi, huyu ndiye mshambuliaji bora zaidi kwa misimu yote mitatu aliyocheza Tanzania Bara. Misimu miwili ameibuka kuwa mfungaji bora na msimu mmoja nafasi ya pili.

Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite kutoka Rwanda wameendelea kuonyesha ni wachezaji wakongwe, lakini ni watendaji hasa wa kazi yao.

BOUBACAR

Wachezaji wawili waliojiunga na Yanga msimu huu, Vincent Bossou na Issoufou Boubacar, hakika bado. Utaona angalau beki Bossou kutoka Togo alienda anaimarika, lakini Boubacar wa Niger, vema akabeba virago vyake na kurejea nyumbani. Kwa kiwango walichofikia Yanga, kama mchezaji wa kimataifa, wanahitaji maradufu zaidi ya huyo.

Simba:
Huku wachezaji bora wa kimataifa walikuwa wa kumulika na tochi, anza na Hamisi Kiiza alifunga mabao 19, mwisho akageuka kuwa mwiba kwa Simba. Uongozi unamtuhumu kuwa mchochezi, lakini yeye amezidi kuonyesha hakuwa akicheza Simba kwa moyo mmoja kwa kuwa wakati akiwa katika vita ya mwisho, kasi ya kufunga ilionekana kupungua, mwisho anaingia kwenye mgomo kwa kucheleweshewa mshahara kwa siku tisa pekee! 

Maana yake alijitoa katika mbio za ufungaji mabao na kuisaidia Simba. Ukiniuliza, mimi nitakuambia naye aende tu, maana hata kocha wa zamani wa Yanga, Ernie Brandts aliwahi kusema, asingependa kumjumuisha katika kikosi chake kama atapewa nafasi hiyo kwa mara nyingine!

KIIZA
Juuko alikuwa kisiki hasa, lakini kila ligi inavyosonga mbele akazidi kulainika. Huenda ndiyo aliingia kwenye figisu kama uongozi wa Simba unavyolalamika au alichoka. Lakini bado anaweza kuwa beki bora akijirekebisha kidogo tu.

Kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast na Mzimbabwe, Justice Majabvi, licha ya kuwa na umri mkubwa lakini walifanya kazi yao kwa ufasaha. Si vibaya kusema walijitahidi sana.

Brian Majwega wa Uganda, Mkenya Raphael Kiongera na beki wa kulia kutoka Burundi, Emiry Nimubona, hawa wangerejea kwao. Hawakuwa na jipya, walijaza tu nafasi za wazawa kucheza huku wakilalamika na kuingia kwenye migomo lakini hakika Simba haikufaidika nao na uchezaji wao wa kiwango cha chini, uliiangusha.

Azam FC:
Iliendelea kubaki timu ya kiwango cha juu, lakini si juu sana. Wageni wengi wanaolipwa vizuri na kupata kila kitu chao vizuri lakini hakuna kubwa sana walilofanya linaweza kuwa tofauti na wazawa hadi wao kuitwa mfano.

Kipre Tchetche, Serge Wawa kutoka Ivory Coast na Jean Baptiste Mugiraneza wa Rwanda, hawa walifanya kazi nzuri. Wako waliojitahidi lakini kundi kubwa wanatakiwa kurejea nyumbani pia.

Racine Diouf, Allan Wanga na Kipre Bolou, hawa wangeweza kutafuta nafasi kwingine. Hata Didier Kavumbagu, vizuri naye angetafuta nafasi kwingine angalau Simba, kwa kuwa inaonekana mfumo wa Azam FC si unaofanana na mwendo wake. Labda kama benchi jipya la makocha vijana kutoka Hispania kama linaweza kumkomboa.

Nyingine:
Timu nyingine zilizokuwa na wageni ni Mbeya City na kipa Mganda, Hannington Kasyebula, Stand United walikuwa na Assouman N’gueassan David kutoka Ivory Coast ambao si wenye kiwango cha juu na unaweza kusema hawastahili kuwa wachezaji wa kigeni wa ligi ya hapa nyumbani, waende kwao.

CHIDIEBERE WAKATI AKIWA STAND 
Coastal Union walikuwa na wageni wawili, Abasrim Chidiebere kutoka Nigeria na Youssuf Sabo raia wa Cameroon. Hawa wameshuka na timu na huenda inawezekana kuzungumza tofauti kwamba Sabo ameonyesha kiwango cha juu kuliko wachezaji asilimia 90 wa kigeni waliocheza Simba. Chidiebere amekwama, lakini msimu mmoja kabla alifanya kweli akiwa na kikosi cha Stand United. Huenda ana uwezo wa kuamka tena na kufanya vema.

Lazima tukubali, wageni sawa. Lakini nafasi kwa wazawa ni muhimu sana. Pia hii inaonyesha kilio cha kuongezewa hadi wachezaji saba wa kigeni, klabu hazijakitumia vizuri kwa kuwa katika saba karibu kila timu imewatumia wageni kwa asilimia ya chini.



2 COMMENTS:

  1. Wageni wapo wachache sana kuliko wazawa....tusiwalaumu sn hao wa kuwalaumu ni wazawa inakuaje mgeni anakuja wakt yupo kawaida alafu anacheza wee mzawa umeridhika kukalia benchi

    ReplyDelete
  2. Wageni wapo wachache sana kuliko wazawa....tusiwalaumu sn hao wa kuwalaumu ni wazawa inakuaje mgeni anakuja wakt yupo kawaida alafu anacheza wee mzawa umeridhika kukalia benchi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic