Na Saleh Ally
SIMBA wameonyesha kuchoshwa na longolongo za Waarabu wa
Etoile du Sahel ya Tunisia na kutengeneza timu ya watu wawili ambayo itafunga
safari kwenda Tunisia ikiongozwa na Rahma Al Kharusi maarufu kama Malkia wa
Nyuki.
Okwi aliuzwa na SImba kwa Etoile du Sahel kwa kitita cha dola
300,000 (zaidi ya Sh 480), lakini hadi leo, Msimbazi wamekuwa wakiendelea
kuangalia hesabu hizo kwenye makaratasi bila ya hata senti moja mkononi.
Timu hiyo huenda ikawa na watu wawili au watatu ambao
wataondoka kwenda Tunisia kuzungumza na uongozi wa Etoile du Sahel kuhusiana na
malipo ya fedha za mauzo ya mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba, zinaeleza timu hiyo
itaongozwa na mlezi wa Simba, Rahma kwenda kukutana na uongozi wa timu hiyo.
“Kweli kuna timu inapanga kuondoka kwenda Tunisia,
inawezekana kabisa kukawa na watu wawili au watatu ila mama (Malkia wa nyuki)
ndiyo ataongoza msafara huo maana tumemuomba afanye hivyo kama atakuwa na
nafasi,” kilieleza chanzo.
“Lengo ni kujaribu kuwahisha suala hilo, maana tunajua Fifa
ina mambo mengi. Uamuzi ulifikiwa kwenye kile kikao cha wiki iliyopita
kilichofanyika pale Serena.”
Awali Watunisia hao waliwaahidi Simba nusu ya fedha hizo
zingetua Dar es Salaam Januari 29 kabla ya kuwamalizia Februari 28, lakini mambo
hayakwenda hivyo.
Uongozi wa Simba ukaamua kuandika barua ukitaka ulipwe zote
ilipofika Februari nao wakakubali, lakini baada ya hapo wameendelea kuwa kimya
hadi Simba walipoamua kuandika barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa).
Barua hiyo imetaka Etoile du Sahel washinikizwe kuilipa Simba
na kama itashindikana basi Okwi arejeshwe nchini na kuendelea kuichezea timu
hiyo ambayo mwendo wake ni wa kinyonga.
Hata hivyo, Malkia wa nyuki ameona suala hilo huenda
likachukua muda mrefu kwa kuwa Fifa ina mambo mengi ya kushughulikia katika
soka na fedha hizo wanaweza wakaona ni kiwango kidogo tu kwao.
Hivyo bora kuwafuata moja kwa moja na kujadiliana nao kuhusiana
na malipo hayo mara moja au kuvunja mkataba wa Okwi ambaye bado alikuwa anahitajika
Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment