May 6, 2016Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita niliandika makala inayohusiana na mimi kutoamini kama kweli Azam FC wamekuwa wakijitoa uwanjani kulingana na namna mwajiri wao anavyojitoa kwao.

Nilieleza namna ambavyo nilikuwa ninaona na kukubali kwamba kweli walikuwa wakijitahidi kufanya kazi yao kwa ushindani na kufanikiwa kutwaa ubingwa pia nafasi ya pili zaidi ya mara mbili.

Nilieleza namna Azam FC ilivyo na wamiliki wenye ndoto kuu za mafanikio na kweli wanajitoa kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri kweli.

Hatujawahi kusikia malalamiko ya mishahara kutoka kwa wachezaji au viongozi pia makocha. Hatujawahi kusikia aliyeachwa Azam FC akilalama mfululizo kwamba hakulipwa. Kila kitu kipo katika utaratibu sahihi.

Angalia uwanja wa mazoezi, angalia uwanja wa mechi, fuatilia wanavyosafiri na kadhalika. Kila kitu safi, lakini bado niliona hawako katika nafasi ambayo wanaweza kumuweka bosi wao katika hali ya kusema, kweli watu wanataka maendeleo hasa na wana tofauti kubwa na timu zinazoishi kwa kuungaunga.

Kabla ya siku nyingi, limeibuka sakata la Azam FC kupokonywa pointi tatu baada ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City.

Inaonekana Azam FC, ilimchezesha beki Erasto Nyoni bila kuangalia kama alikuwa ana kadi tatu za njano. Haya ni mambo ambayo yalikuwa yanafanya tuone mchezo wetu wa soka una mambo ya kubabaisha sana kwa kuwa Yanga na Simba, wameyafanya sana.

Kweli binadamu tunakosea, hili nalikubali lakini kweli hesabu ya kadi kuanzia moja mpaka tatu inaweza kuwa ngumu. Kila mmoja anajua kuna uwekaji wa takwimu na zina matumizi yake, vipi meneja wa Azam FC au mhusika wa hilo hakulifanyia kazi kwa umakini?

Mimi nimeona ni kero kubwa ambayo inapaswa iwe mwisho ili tuachane na mwendo huo ambao kwetu tumekuwa tukiuona tatizo kubwa kwa kuwa inaonekana soka, watu wake ni wale wanaobahatisha mambo.

Azam FC imeingia kwenye kero ya wiki na sasa inapambana na ile kero ya wimbo wa ‘Chura’ ambao Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limetangaza kuufungia na pia kumsimamisha kufanya kazi za muziki msanii Snura Mushi.

Snura tayari amejipu mapigo, huenda atakuwa na hoja zake lakini ukweli kabisa wimbo ule haupendezi kuwa sehemu ya jamii na kila mmoja anaona.

Waliocheza video ya wimbo huo ambayo ilikuwa inasambazwa mitandaoni nao waliziba sura zao kwa kuwa waliona haya au aibu. Walijua kabisa wanachofanya si sahihi kwa jamii.

Snura ameomba radhi lakini akazungumza mambo mengi ya kijinga. Moja ni kusema hakuamini kama watoto wanaweza kuingia mtandaoni na kuiona.

Mimi naamini ameamua kuichezea jamii, ameamua kutoa video hiyo akiamini si sahihi, atakuwa gumzo, atapata ‘kiki’ ataamka na baada ya hapo ataomba radhi, jambo ambalo naliona si jema kwa jamii.

Nilizoea kumuona Snura akiwa anaongozana na Wema Sepetu aliyekuwa rafiki yake mkubwa. Haijapita hata miaka mitatu na wakati huo hakuwa akiimba, lakini tayari sasa Snura anataka kuwa msanii mkubwa hata kuliko Hassan Bichuka. Ikishindikana, ndiyo hivyo analazimisha mambo.

Ninaamini akiendelea hivi, uhai wake kimuziki, hautakuwa na muda mrefu, ataanguka na hatarejea tena.

Snura na benchi la ufundi la Azam FC, kwangu ndiyo watu waliochafua upepo wa michezo upande wa soka, pia upande wa burudani katika muziki wa kizazi kipya.
Nasisitiza, kama binadamu kukosea ni jambo lipo. 

Kuna haja ya kuangalia unakosea wapi na inakuwa vipi.

Kufanya makusudi utoke ili uombe radhi, au kufanya uzembe wakati wenzako wakipigania jambo kama ilivyo kwa Azam FC, ni kitu kibaya na kinastahili adhabu. 

3 COMMENTS:

  1. mambo ya kawaida hayo, real madrid mbona walitolewa kwenye kombe la mfalme kwa kosa kama hilo. au sababu imetokea Bongo?

    ReplyDelete
  2. Nyie si ndio mliodai eti AZAM imekuja kuleta mageuzi ya soka Tanzania sasa vipi tena?Sasa hayo ni mageuzi ya kanuni za soka ndio AZAM wamezileta,hakuna kitu hapo!

    ReplyDelete
  3. Kumbe kadi za mechi ya ngao ya hisani huwa zinaunganishwa kwenye mechi ya ligi kuu ya Vodacom?inawezekana benchi la ufundi la Azam hawakuwa na uelewa wa suala hili,hivyo ni fundisho la kikanuni kwa familia ya soka.Hivi kuna rufaa iliyokatwa na Mbeya City au tu watu wamekaa ofisini wakatengeneza malalamiko kwa manufaa yao?Mbona hatukusikia Mbeya City ilikuwa imekata rufaa baada ya mechi hiyo?na kwa nini uamuzi huo unafanyika sasa zaidi ya miezi miwili tangu tukio lilipotokea?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV