May 28, 2016


Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amepania kulichukua Kombe la Shirikisho Afrika, kwani amepanga kutokubali kufungwa kwenye mechi zote za ugenini ikiwemo dhidi ya TP Mazembe. 

Hiyo ni baada ya juzi na jana kukaa na kuweka mikakati ya jinsi ya kulichukua taji hilo baada ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho waliyoingia kwa kuwatoa Sagrada Esperanca ya Angola.

Yanga ipo kwenye Kundi A na timu za MO Bejaia ya Algeria, Medeama (Ghana) na TP Mazembe ya DR Congo. Kundi B zipo Kawkab na FUS Rabat zote za Morocco, Etoile du Sahel (Tunisia) na Ahly Tripoli ya Libya.

Pluijm amesema ushindi wa ugenini unaifanya timu pinzani kucheza kwa presha kubwa katika mchezo wa nyumbani, hivyo amepanga kutumia mbinu hiyo akiamini itampa taji hilo.

Pluijm alisema, amefikia hatua hiyo baada ya tathmini aliyoifanya kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwani walifungwa michezo miwili ya ugenini dhidi ya Al Ahly mabao 2-1 na Esperanca bao 1-0.

“Timu yetu ina rekodi mbaya ya kufungwa mechi za ugenini na hilo nimeliona kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo sitaki kuliona hilo likijitokeza kwenye Kombe la Shirikisho.

“Nitakachokifanya ni kupambana kwenye mechi zote tutakazozicheza ugenini kwenye hatua hii ya makundi Kombe la Shirikisho, kuhakikisha tunashinda ili kuwapa mazingira magumu wapinzani wetu kwenye michezo ya nyumbani.

“Hiyo tathmini nimeifanya kwenye Ligi ya Mabingwa kwani tulipata matokeo mazuri nyumbani pekee na ugenini tukafungwa, hivyo sitaki kuona tukiendelea hivi.

“Naendelea kukiboresha kikosi changu kuhakikisha tunachukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho, lengo ni kuzima utawala wa Mazembe,” alisema Pluijm.

Katika rekodi zake, TP Mazembe imetwaa mara tano ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika miaka ya 1967, 1968, 2009, 2010 na 2015, pia imetwaa mara moja Kombe la Washindi (sasa Kombe la Shirikisho) mwaka 1980. Yanga haijawahi kutwaa ubingwa wowote wa Afrika.

Mtanzania Thomas Ulimwengu ni miongoni wa wachezaji tegemeo wa TP Mazembe hivi sasa.

Yanga itaanza mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho kati ya Juni 17 hadi 19, mwaka huu kwa kucheza na Mo Bejaia ya Algeria ugenini halafu itaikaribisha TP Mazembe nyumbani kati ya Juni 28 na 29.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV