May 16, 2016


Ikiwa imetoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga itapambana na Sagrada Esperanca ya Angola keshokutwa Jumatano lakini kocha Hans van Der Pluijm ametahadharisha kuwa Waangola hao wataumia vibaya kama wakija kichwakichwa kwa kuwa kikosi chake bado kina morali kubwa ya ubingwa.

Yanga imeondoka Dar leo alfajiri kwenda Angola kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho wakiwa na hazina ya mabao 2-0 waliyoyapata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar siku chache zilizopita. Wakisonga mbele wataingia kwenye hatua ya makundi.

Pluijm amesema: “Tunaenda kupambana kwani tunafahamu kwamba wapinzani wetu watakuwa na mbinu mpya ya kuona wanawezaje kukomboa mabao yale na kututoa mashindanoni.
“Hiyo haitakuwa kazi rahisi kwani na sisi tumejipanga kuhakikisha tunafuzu hatua ya makundi, hivyo basi naamini mchezo utakuwa mzuri sana.

“Pia natambua kwamba mechi ya nyumbani si sawa na ya ugenini, tulicheza vizuri nyumbani tukapata matokeo na hivyo wao watakuja na mbinu za kutaka kutushambulia muda wote ili kuwanyima fursa mabeki wangu kupanda mbele na kutengeneza mashambulizi.


“Kama wakija na mbinu hiyo wataumia vibaya kwani tayari nimelifanyia kazi suala hilo, kikubwa tutacheza kama kawaida yetu staili ya kutumia mabeki kupandisha mashambulizi na kupiga krosi, naamini hiyo itawafanya wapunguze kasi ya kuja golini kwetu na kuanza kujilinda, hapo ndipo tutakuwa tumewaweza.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV