May 27, 2016Juzi Kocha wa Simba, Jackson Mayanja alikabidhi ripoti yake kwa Kamati ya Ufundi iliyokuwa ikieleza mabadiliko mengi katika kikosi hicho iliyohitaji kutema na kutoa wachezaji wengi kwa mkopo kwa ajili ya kuongeza sura mpya zitakazoleta heshima ya Wekundu hao msimu ujao.

Ripoti hiyo ambayo ilijadiliwa kwenye moja ya ofisi za vigogo wa timu hiyo imeonyesha kuhitaji kuondolewa kwa wachezaji wote wa kigeni isipokuwa kipa Muivory Coast, Vincent Angban.

Mzimbabwe, Justice Majabvi ambaye yeye ameomba kuondoka baada ya msimu huu kutokana na udhuru wa kuungana na mkewe nchini Australia, ripoti hiyo imesisitiza kuwa kiungo huyo asiondoke klabuni hapo kabla ya Simba kuhakikisha imempata mbadala wake mwenye uwezo mkubwa zaidi katika eneo la kukaba.

Mtu wa ndani kutoka Simba amesema wengine waliobaki, wakiwemo Waganda, Hamis Kiiza, Juuko Murshid, Brian Majwega, Mkenya, Paul Kiongera na Mrundi, Emery Nimubona wao wamepigwa panga kwa sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu na wengine viwango duni.

Pamoja na hayo, baadhi ya wachezaji waliopendekezwa kuachwa kikosini hapo ni pamoja na Mohammed Fakhi na Hassan Isihaka huku Said Ndemla akihitajika kutolewa kwa mkopo kulingana na kiwango duni alichokionyesha msimu huu.

Hata hivyo, suala la Ndemla liliibua mgongano wa mawazo na mwisho likajumuishwa kwenye viporo ambavyo vitakwenda kujadiliwa na kamati hiyo kisha kutolewa majibu siku za usoni.

“Yamejadiliwa mengi sana katika usajili lakini kuna vitu vinahitaji kujadiliwa zaidi, hivyo kamati itakuja na majibu, ukiachana na wanaopunguzwa lakini wapya watakaosajiliwa kuibeba timu wamelengwa zaidi kuwa ni wachezaji wa kimataifa, hivyo usajili wao utatolewa macho zaidi,” kilieleza chanzo hicho.

Alipotafutwa Mayanja kutolea ufafanuzi wa kina ripoti hiyo, alisema: “Siwezi kukwambia ripoti ilivyokuwa lakini nikwambie tu kwamba asilimia kubwa ya wageni walioonekana hawana msaada na wanaididimiza Simba hao wataondoka.

“Wachezaji wa ndani nao wataangaliwa kulingana na walichokifanya msimu uliopita. Unajua Simba ya sasa haihitaji tena mpira wa kucheza na jukwaa pekee bali mtu anayeweza kuleta matokeo katika kila mechi na mwenye msimamo wa juu wa kiwango chake kwa muda wote.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV