Siku moja baada ya Yanga kufanikiwa kunyakua ubingwa Kombe la FA, straika Mrundi, Amissi Tambwe, amesema yupo tayari kurudi Simba kama uongozi wa timu hiyo utamhitaji.
Hata hivyo, Tambwe ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu na ambaye pia juzi Jumatano aliiongoza Yanga kuifunga Azam FC mabao 3-1, katika mchezo wa fainali wa Kombe la FA alisema kuwa atafanya hivyo mara tu uongozi wa Simba utakapomuomba radhi kwa mabaya yote uliyomfanyia wakati akiitumikia klabu hiyo.
Tambwe alisema licha ya kuwa na furaha Yanga lakini anaionea huruma Simba ambavyo inataabika kuhakikisha inarudisha makali yake.
Alisema kitendo hicho kimekuwa kikimsononesha kwani hakutarajia kama ingekumbwa na hali hiyo kutokana na jinsi viongozi wa timu hiyo walivyokuwa wakijisifu baada ya kumfungashia virago kwa mbwembwe.
“Pamoja na yote hayo mimi huwa sina kinyongo kwani walifanya hivyo bila kujua nini kitatokea mbele yao na sasa najua watakuwa wanajuta kwa uamuzi wao huo wa kunifukuza klabu kwao.
“Hata hivyo, naomba kuwaambia kuwa kama wananihitaji na wanataka nirudi klabuni hapo basi waniombe radhi kwani walinidhalilisha sana, wakifanya hivyo mimi nipo tayari kurudi lakini nitakapomaliza majukumu yangu na klabu yangu ya Yanga ambayo inanithamini na ninaishi kwa amani,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment