Kocha wa Makipa wa Yanga, Juma Pondamali, amemjia juu kipa wake, Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya kipa huyo mara kwa mara kufanya makosa ya kizembe ambayo huwapa wapinzani wao mabao ya mapema.
Pondamali ameweka wazi kuwa kwa siku za hivi karibuni, Dida amekuwa hana umakini anaposimama langoni na kufanya makosa ya kizembe, hivyo ameanza kumchunguza ili kubaini tatizo lake kwa kina.
Pondamali amesema kuwa makosa anayoyafanya Dida ni hatari sana kama watakutana na timu inayoweza kutumia makosa ya kipa, hivyo anafanya juu chini kutibu tatizo hilo kwani kama akimuacha anaweza kuwagharimu kwenye mechi zijazo na kuwafanya wakose ubingwa.
“Sielewi ana tatizo gani kwani kwenye mechi kama tatu mfululizo namuona hana umakini kabisa, mechi ya Coastal Union alifanya uzembe tukafungwa bao na kutupa shida ya kuchomoa na kuongeza, pia ile ya JKT Mgambo akafanya makosa yaleyale.
“Hii ni hatari kwetu kwa kipindi hiki tulichopo cha kusaka ubingwa, mpaka wakati mwingine namuuliza Dida unataka kuniua na presha maana simuelewi nini malengo yake ya anachokifanya, hivyo ni lazima nikae naye na kumchunguza nini kinamsibu mpaka kipindi hiki apoteze umakini golini, kikubwa kwa sasa tunataka ubingwa na si kingine,” alisema Pondamali.
0 COMMENTS:
Post a Comment