May 28, 2016Na Saleh Ally
UKISIKIA mashabiki au viongozi wengi wa Simba wanazungumza kuhusiana na kutobeba ubingwa katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2015/16 uliomalizika siku chache zilizopita, utagundua lawama inachukua nafasi kubwa sana.

Utasikia ‘tulionewa’, Yanga ‘walipendelewa’, TFF ‘haitupendi’ na kadhalika. Hakuna hata mmoja anayekubali kuainisha makosa ya msingi ya Simba ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi.

Simba iliyoshika nafasi ya tatu, inapaswa kujiimarisha zaidi kuliko kulalamika zaidi kwa kuwa mambo mengi yalikuwa ni makosa ya wachezaji na makocha na uongozi nao kwa kuwa unafanya usajili, lazima wakubali makosa yanayowahusu halafu wafanye haya yafuatayo;

Washambuliaji:
Simba ilikuwa na safu ya tatu kwa ubora wa ufungaji mabao ingawa ilikuwa na nafasi kubwa kushika nafasi ya pili kama washambuliaji wake wangekuwa makini mwishoni.
 Simba imemaliza ikiwa na mabao 45, Azam FC ya pili ikiwa na 47 na utaona tatizo linajengwa na tofauti ya Yanga ambao wamekuwa mabingwa na vinara wa kufunga mabao mengi baada ya kupachika 70 katika mechi 30 kama zile za Simba.

Hamisi Kiiza amefunga mabao 19, huenda angefunga mengi zaidi kama angekuwa ni mchezaji mwenye aina ya Amissi Tambwe. Mtu mwenye nidhamu ya juu ndani na nje ya uwanja.


Mwishoni aliingia kwenye matatizo na uongozi, mara zaidi ya moja. Hii ilichangia yeye kuondoka kwenye mchezo na huenda asingeweza kufanya vizuri zaidi.
Lakini Simba ilionekana kwenye ushambuliaji ina uwezo wa kusimamia mguu mmoja. Kama hayupo Kiiza, basi na inawezekana kabisa hii ilichangia ‘kumchechetua’ Kiiza kujiona hakuna kama yeye na kuingia kwenye malumbano na meneja wa timu aliyefikia hatua ya kumtimua kambini. Siku chache, akaingia kwenye mgomo, akaondolewa kambini tena.

WAFANYE HIVI: Lazima Simba sasa iinue macho, Kiiza hakuwa mshambuliaji wa kutisha sana (angalia rekodi zake Yanga), lakini Simba alifanya vema kutokana na muunganiko wa kikosi. Kama watapata mshambuliaji sahihi, nafasi ya kufanya vizuri ipo kubwa sana. Hapa lazima Simba waepuke ubahili.

Viungo:
Simba haikuwa na tatizo kubwa la viungo lakini kama Justice Majabvi ameomba kuondoka, uongozi uliangalie hili haraka na kutafuta kiungo hasa, mtu hasa ambaye atasimama akiwa imara kweli na pia uzoefu.

WAFANYE HIVI: Jonas Mkude anaweza kucheza vizuri, lakini lazima kuwe na kiungo mzoefu zaidi. Au acheze namba nane, au awe namba sita Mkude apande. Lakini bado Simba inatakiwa kuwa na kiungo wa pasi za mwisho kwa kuwa msimu ulioisha haikuwa na mtu mahiri katika anga hizo.


Beki wa Kati:
Juuko Murshid ndiye aliongoza jahazi na hadi mwisho wa ligi, kitakwimu Simba ndiyo yenye safu bora zaidi ya ulinzi Ligi Kuu Bara. Imemaliza mechi 30 ikiwa imefungwa mabao 17.

Mabingwa Yanga walifungwa 20 na Azam FC 24. Lakini mwishoni, Juuko akaonekana kudorora na watu wakawa wanapita tu.

Bado beki kama Novatus Lufunga ni mzuri, lakini bado anahitaji muda hivyo vizuri acheze chini ya kiongozi sahihi.
WAFANYE HIVI: Simba lazima wasajili mabeki wazoefu na wakubali, sehemu ya kati ya ulinzi si ya kufanyia mafunzo na kukuza vijana hasa wakati wa presha kama waliyonayo sasa. Misimu minne sasa wamekuwa wakikuza tu na hakuna faida. Beki mwenye uzoefu ni muhimu sana.
Kama Juuko atabaki, lakini kunatakiwa beki mwingine nguli hasa ambaye pia ikiwezekana ‘wavunje benki’.

Beki wa Kulia:
Baada ya kuondoka kwa Hassan Kessy na Simba kutoridhishwa na kiwango cha Emiry Nimubona, hili ni tatizo jingine kubwa.

Siku hizi, mabeki si walinzi pekee badala yake ni mabawa ya ushambulizi.

Angalia Shomari Kapombe na Juma Abdul walivyozisaidia Azam FC na Yanga.

WAFANYE HIVI: Simba inahitaji mtu sahihi na mahiri, kubahatisha katika nafasi hii ni kuendelea kuuota ubingwa na kutegemea kubahatisha ili kuupata.
Kushoto, Simba haina shida kubwa lakini Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ pekee pia bado hafai. Hakuna haja ya Simba kuona kuondoka kwa Kessy si pigo au pengo, badala yake walifanyie kazi hilo kwa uhakika.

Kipa:
Kipa mmoja wa uwezo wa asilimia 65 ambaye anaweza kuimarika zaidi Simba, anahitajika. Maana Vincent Angban alionyesha uwezo wa juu kabisa huenda kuliko makipa wote wa Tanzania Bara. Utaona hata safu yake ya ulinzi imekuwa bora zaidi.

WAFANYE HIVI: Manyika Peter pamoja na kupewa mechi chache, bado alikuwa bora. Kuongezwa kwa kipa mmoja, kutaongeza tu upinzani, lakini hapa Simba, hawako vibaya sana. Ila kipa huyo atakuwa akiba iwapo Angban kaumia au kupumzishwa na yeye na Manyika, wataongoza jahazi.

Benchi la Ufundi:
Inaweza ikawa kuna ugumu Simba kukubali lakini benchi lao la ufundi lilikuwa hovyo kabisa, hili walijue kwa mara nyingine.

Hadi mwisho wa ligi, liliongozwa na kocha msaidizi ambaye hakika alijitahidi sana. Lakini pamoja na kuwa msaidizi Jackson Mayanja hakuwa na usaidizi sahihi.

Hakuwa na kocha msaidizi wa kiwango cha kukaa katika benchi la Simba. Hakuwa na kocha wa makipa sahihi anayeweza kuwa na kiwango cha Simba, huenda wengine walikuwepo kwa kuangalia suala la mapenzi.

WAFANYE HIVI: Simba kama inataka mafanikio, lazima iwe na kocha bora wa makipa, msaidizi sahihi mwenye ‘levo’ ya Mayanja lakini ijiulize, vipi kuhusu kocha wa viungo, wataalamu wa chakula na kadhalika?


Simba ni timu kubwa inayohitaji kwenda mwendo sahihi utakaoifanya bora. La sivyo, itaendelea kubahatisha. Kikubwa zaidi, kama inaongeza kocha lazima imshikilie Mayanja ambaye ameonyesha bora akiwa nao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV