Lile shindano bab’kubwa linalowakutanisha vijana kutoka pande mbalimbali za Afrika Mashariki lijulikanalo kwa jina la Maisha Plus East Afrika, limekuja tena na sasa linaingia msimu wake wa tano.
Shindano hilo lililoanzishwa mwaka 2008, lina lengo la kuwakutanisha vijana na kuishi maisha halisi ya kila siku Watanzania na watu wa Afrika Mashariki kwa jumla ambapo jana Ijumaa ndiyo uzinduzi wake ulifanyika kwenye Ofisi za Kampuni ya Azam Media zilizopo Tabata jijini Dar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DMB ambayo ndiyo waandaaji wa shindano hilo, Masoud Kipanya, amesema msimu huu utakuwa ni wa tofauti sana kuliko misimu yote iliyopita, mbali na yote hayo pia zawadi za mshindi wa kwanza zimeongeza.
Kipanya amesema kila msimu wamekuwa wakiongeza shilingi milioni tano ili kuongeza motisha, hivyo baada ya msimu wa kwanza mshindi kuondoka na shilingi milioni 10, sasa mshindi atajinyakulia shilingi milioni 30.
“Msimu wa tano wa Maisha Plus umezinduliwa leo (jana) na tunatarajia Jumapili hii kuanza kuonyesha vipindi vya nyuma huku tukianza mchakato wa kuwasaka washiriki wa msimu huu.
“Niwaambie tu msimu huu ni wa kipekee, washiriki wanapaswa kuendana na kile kinachotakiwa kufanyika ndani ya kijiji ambacho hatuwezi kukiweka bayana lakini ndicho kitwakutanisha vijana wetu hao na kuishi humo kwa takribani miezi mitatu.
“Washiriki watakuwa 30 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ambapo kati ya washiriki hao 30, wanaume watakuwa 15 na wanawake 15,” alisema Kipanya.
Naye Mkurugenzi wa Azam TV ambao ndiyo kituo cha runinga kitakachoonyesha shindano hilo mwanzo mpaka mwisho, Tido Mhando, amesema wao kama Azam wanajisikia faraja kuonyesha mashindano hayo ambayo yamekuwa kivutio kwa watazamaji tangu kuanzishwa kwake.
Baada ya mchakato wa kuwapata washiriki kukamilika, shindano hilo linatarajiwa kuanza rasmi Juni 17, mwaka huu na kufikia tamati Septemba, mwaka huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment