May 28, 2016



Straika wa Yanga, Donald Ngoma, amesema mabeki Juuko Murshid wa Simba na Pascal Wawa wa Azam FC ni wepesi kwake kuliko wale wa Coastal Union ambayo imeshuka daraja.

Juuko ndiye aliyeiongoza safu ya ulinzi ya Simba ambayo imefungwa mabao machache katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kuruhusu mabao 17 tu, Wawa yeye anatajwa kwa uhodari wake wa kuzuia.

Ngoma ambaye alifunga mabao 17 katika ligi hiyo, amesema kuwa, mabeki wa Coastal Union walikuwa wakimpa tabu alipokutana nao katika mechi ya ligi na Kombe la FA.

“Coastal Union ndiyo timu iliyokuwa na mabeki hatari sana kwangu, walinizuia kupita kiasi na kila nilipokutana nao ilibidi nitumie akili ya ziada zaidi kwani wanacheza kwa kujituma sana.

“Nimekabwa na mabeki tofauti kwenye msimu huu wa ligi kuu wakiwemo wa Simba na Azam, lakini kwa safu ya ulinzi ya Coastal Union ni kiboko kutokana na aina yao ya uchezaji.

“Mabeki wao wanacheza kwa nidhamu kubwa ndani ya uwanja, pia wana fiziki ya kutosha hivyo ukitaka kugongana nao, basi unatakiwa ujiandae kwelikweli.

“Walinifanya nitumie muda mwingi kupanga kila aina ya mbinu za jinsi ya kuwatoka ili nifunge kutokana na ubora wao, hivyo kwa upande wangu ni timu yenye safu nzuri kwa timu pinzani,” alisema Ngoma.

Mabeki anaozungumzia Ngoma raia wa Zimbabwe ni Hamis Mbwana, Abdulhalim Humud ambaye awali alikuwa akicheza kama kiungo akiwa amewahi kucheza Simba na Azam.

Yanga imekutana na Coastal Union mara tatu msimu huu, katika ligi kuu Yanga ilishinda mabao 2-0, halafu ikafungwa mabao 2-0 na katika nusu fainali ya Kombe la FA, Wanajangwani walishinda mabao 2-1.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic