June 13, 2016Na Saleh Ally
HAKUNA anayeweza kukataa kwa msimu uliopita wa 2015/16, Juma Abdul Jaffar ambaye jina lake la ukoo ni Mnyamani, ndiye aliyekuwa beki bora kabisa wa kulia.
Mnyamani, ameonyesha uwezo mkubwa na kutoa mchango wa juu ulioiwezesha Yanga kubeba makombe yote ya msimu huo. Yaani ubingwa wa Bara na ule wa Kombe la Shirikisho maarufu kama Kombe la FA.

Pamoja na hivyo, ameisaidia Yanga kwa ufanisi mkubwa kufika katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho, kazi ambayo wataianzia nchini Algeria, wiki hii.

Beki huyo, ndiye aliyeongoza kwa kutoa pasi nyingi zaidi za ufungaji mabao kutokana na krosi ‘chumba na sebule’ alizokuwa akizimimina. Amefanikiwa kumaliza msimu akiwa na pasi 14 zilizozaa mabao, pia mabao matatu aliyofunga mwenyewe kupitia mikwaju yake mikali katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

JUMA AKIWA NA RAFIKI YAKE AMBAYE WANAISHI PAMOJA.
SALEHJEMBE ilifika nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam na kufanya naye mahojiano.

SALEHJEMBE: Yanga imeondoka, wewe unabaki kwa kuwa majeruhi, nini tatizo?
Mnyamani: Nimepata tatizo kwenye mfupa wa mguu hapa, jamaa alinigonga katika mechi dhidi ya Misri. Daktari kaniambia mfupa mdogo umechanika.

SALEHJEMBE:  Lini utarejea?
Mnyamani: Kasema nitaendelea na matibabu kwa wiki moja na nusu, halafu nitaanza mazoezi ya taratibu. Ila ninaweza kuanza mapema kutegemeana na kupona.

SALEHJEMBE:  Ulianzia Mwanza United, Toto African na baadaye Mtibwa Sugar. Lakini unaonekana ni mwiba ukiwa Yanga, nini kilichokubadilisha?
Mnyamani: Kweli nimebadilika kwa mengi, labda nifafanulie zaidi.

SALEHJEMBE:  Unapiga mashuti makali sana, haikuwa hivi kabla?
Mnyamani: Kweli nikiwa Yanga kiwango kimepanda. Lakini mashuti mimi ni kipaji changu ingawa nikiwa Yanga nimejiimarisha zaidi kwa mazoezi.

SALEHJEMBE:  Vipi kuhusu krosi?
Mnyamani: Krosi inategemeana na mfumo. Lakini pia ni kitu ninachokifanyia sana mazoezi. Kocha (Hans van Der Pluijm) anasisitiza suala la ulinzi kwa mabeki. Kwenda kushambulia ni muhimu, lakini pumzi na stamina yako ndiyo itakuongoza.
SALEHJEMBE: Wewe unaweza vipi vitu vyote kwa wakati mmoja?
Mnyamani: Ni kazi ngumu sana kaka, lakini niamini ninafanya mazoezi mengi sana ya ziada ili niwe fiti zaidi.

SALEHJEMBE:  Wakati unaingia Yanga mwaka 2012, ulicheza mechi chache kuanzia Kombe la Kagame hadi ligi, mara nyingi ulikuwa majeruhi. Tatizo lako lilikuwa lipi?
Mnyamani: Kwenye Kagame niliumia nusu fainali, mechi dhidi ya APR, aliniumiza Twite (Mbuyu). Kwenye ligi kweli nilicheza mechi chache sana. Kuumia mara kwa mara kuliniponza.

SALEHJEMBE:  Kuumia mara kwa mara ni kutokuwa fiti, ulikuwa na tatizo lipi? Warembo au pombe?
Mnyamani: Mimi pombe sinywi, sema starehe na kutopumzika. Dar es Salaam ni kwetu lakini siku nyingi sikuwepo, hivyo nilikuwa kama ndiyo naingia mjini, ikawa shida tu.

SALEHJEMBE:  Nini kilikubadilisha?
Mnyamani: Nilishituka na kujitambua, niliona Yanga ina wachezaji wengi wanaojua mpira lakini wameondoka kwa kushindwa kujitambua. Nikaamua kubadilika na kuanza kufanya mazoezi ya ziada, imenisaidia sana kuwa fiti. Nilianza kwenda Coco Beach mchangani, halafu gym pale Kijitonyama. Wakati mwingine kabla ya mazoezi ya timu, mimi ninafanya yangu ya kutosha kabisa.

SALEHJEMBE:  Sasa una ushindani, kuna Hassan Kessy kutoka Simba, hii haikupi hofu?
Mnyamani: Mimi si mtu wa hofu, ninapenda ushindani. Pia Kessy ni mchezaji mzuri, hivyo atanipa morali ya kupambana zaidi kwa kuwa nataka kubaki kikosi cha kwanza niisaidie Yanga.

SALEHJEMBE:  Ukiambiwa umshauri Kessy kwa kuwa yuko Yanga, utamweleza nini?
Mnyamani: Kwanza kumkaribisha na kumueleza Yanga si Simba, mfumo wake ni tofauti. Lazima ajitume na pia nidhamu ya huku iko juu sana. Vizuri sana akajitambua na mambo yatakuwa mazuri kwake.

SALEHJEMBE: Una ndoto za kucheza nje ya Tanzania? Labda nchi gani?
Mnyamani: Kabisa, nchi sijui lakini hata ikiwa nje hapa Afrika katika timu kubwa Al Ahly, TP Mazembe au timu nyingine kubwa za Afrika Kaskazini. 

SALEHJEMBE:  Msimu uliopita, mmewafunga Simba mara mbili, unafikiri mnaweza kuendeleza hili msimu ujao?
Mnyamani: Ndiyo, inawezekana kabisa. Yanga tuko vizuri na msimu uliopita kama tungekuwa makini hata tano tungewafunga, hawakuwa vizuri.

SALEHJEMBE:  Nani alikupa shida zaidi ulipokabana naye msimu uliopita?
Mnyamani: Kipre (Tchetche) wa Azam FC, mjanja na ana kasi. Ukikutana naye unalazimika kujiandaa sana. Mwingine ni Farid (Mussa) pia wa Azam, dogo ana kasi sana pia. Lazima uwe sawa sana kumdhibiti.

SALEHJEMBE:  Unapocheza Taifa Stars, kidogo wingi wa krosi unapungua sana, vipi ni woga?
Mnyamani: Hapana, kidogo mifumo inapishana. Utaona Ulimwengu (Thomas) anapokuwa juu ni tofauti na tunapocheza na Msuva (Simon) Yanga. Hivyo mambo yanabadilika.

SALEHJEMBE:  Yanga imevuka hadi robo fainali Kombe la Shirikisho, unafikiri mtafika mbali na kwa nini?
Mnyamani: Mimi ninaamini tuna kikosi bora, tutafika mbali. Ni wachezaji kujituma, viongozi waungane na sisi na kutupa sapoti pia mashabiki.
Kama tumevuka Angola ambako ilikuwa ni lazima tufungwe. Vipi tushindwe kupita? Tujiamini na kupendana pia kama mwanzo, tutapita.

SALEHJEMBE:  Jina lako limepanda sana midomoni mwa wapenda soka, vipi mashabiki wanapokuona mtaani?
Mnyamani: Kweli wananifurahia sana, wanataka angalau hata kuzungumza kidogo tu na mimi. Hii inanipa sana faraja na kunifanya niongeze juhudi zaidi.

SALEHJEMBE: Unaishi Sinza, unajua tena kwa wajanja. Unaepuka vipi vishawishi kwa warembo?
Mnyamani: Nina mtu wangu, huenda akawa mke wangu Mungu akijaalia. Hivyo ninaye, pia najitahidi kuwa ni mtu mwenye kufuata misingi. Angalia kina Samuel Eto’o walitafuta, sasa wanakula kwa raha. Starehe zipo tu, sasa ni kutafuta kwanza kwa uhakika.

SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV