August 19, 2016

Mshambuliaji wa timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, usiku wa kuamkia leo aliiongoza timu yake kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Locomotiva Zagreb ya Croatia.

Katika mchezo huo wa hatua ya mtoano wa Kombe la Europa uliochezwa kwenye Uwanja wa Maksimir jijini Zagreb, Samatta Ambaye ni Mtanzania alifanikiwa kufunga bao moja lakini bado timu yake ina kazi kwa kuwa timu hizo zitarudiana Alhamisi ijayo. 

Timu hiyo ya Samatta itatakiwa kupata ushindi wowote au sare ya bao 1-1 ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwa ajili ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ambapo huko ndipo watakapokutana na vigogo wengine wa Ulaya wakiwemo Manchester United.

Samaata alifunga bao lake katika dakika ya 47 wakati lile la kwanza liliwekwa wavuni ni Leon Bailey katika sakika ya 35 kwa njia ya penalti.

Kuongoza kwa mabao 2-0 kuliwafanya Genk waamini kuwa mwamemaliza kazi lakini wenyeji walisawazisha kupitia kwa Mirko Marić kwa njia ya penalti dakika ya 52 na dakika ya 59 goli likifungwa na Ivan Fiolić.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana tena Agosti 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Cristal Arena unaomilikiwa na KRC Genk.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV