August 3, 2016



Na Saleh Ally
MFANYABIASHARA bilionea kijana Mohammed Dewji maarufu kama Mo, ametangaza kuwekeza katika Klabu ya Simba kwa kutoa Sh bilioni 20 ili amiliki hisa kwa asilimia 51, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wanachama wa Simba.

Lakini limekuwa gumzo hata kwa wapenda michezo wengi kuhusiana na namna ambavyo suala hilo linakwenda, kwamba je, Simba wanapaswa kuingia kwenye mabadiliko au la?

Mashabiki na wanachama wengi wa Simba, wanaonekana wazi wanachotaka ni mabadiliko na kwa asilimia kubwa wameanza kuushinikiza uongozi wa timu hiyo kuhakikisha unaingia kwenye mabadiliko hayo kwenda kwenye kampuni na baadaye mfumo wa hisa uanze kutumika.

Baadhi ya wanasiasa, nao wameonekana kuunga mkono ingawa wamekuwa na mawazo tofauti lakini msisitizo kuwa ni wakati mwafaka kwa Simba kuingia kwenye mabadiliko hayo.

SALEHJEMBE:, ilifanya juhudi za kumpata Mo Dewji ili kuzungumza naye kuhusiana na suala hilo ili kujua maoni yake kwa undani zaidi na nia yake hasa.

SALEHJEMBE: Sh bilioni 20 si fedha kidogo, nini hasa kitakufaidisha wewe kama mfanyabiashara kuingiza fedha hizo ndani ya Simba?
Mo: Niseme ni suala la kujiuliza lakini jibu la kwanza nitakuambia ni mapenzi yangu kwa Simba. Lakini ninaamini nitakaposhirikiana na wanachama na mashabiki wa Simba, tutakwenda kwenye mabadiliko na kuifanya Simba kuwa klabu bora ambayo ina uwezo wa kushindana barani Afrika na mwisho mafanikio yatapatikana.

SALEHJEMBE: Unaamini kinachosababisha hivi sasa kuyumba kwa Simba ni fedha peke yake?
Mo: Lazima uwekeze fedha ndiyo ufanikiwe. Lakini lazima uwekeze mfumo kwa ajili ya kuziendesha kwa mwendo sahihi hizo fedha. Simba haiwezi kushindana tena na Yanga na Azam FC kwa kuwa haina fedha. Wao wanafanya mambo mazuri, wanasajili kwa uhakika, kambi bora, huwezi kuwashindanisha na Simba.

SALEHJEMBE:Umesema unatoa Sh bilioni 20, halafu unapenda kuweka bond na baada ya hapo Simba itatumia faida ya hiyo bond kujiendesha. Sasa fedha unayotumia inakuwa ni ile uliyonunulia, huoni hapo unapata faida mara mbili?
Mo: Fedha hiyo ni ile ya Simba, bado inaweza kutumika kwenye maendeleo. Mimi pia ninaweza kuwekeza zaidi. Pia kumbuka fedha hiyo ya Simba itakuwa salama itakapokuwa kwenye ‘treasury bond’. Usipoiweka kule italiwa na mwisho itakuwa Simba ndiyo imepoteza.


SALEHJEMBE: Umepanga kutoa Sh bilioni 20 upate asilimia 51, una uhakika fedha hizo ni sawa na thamani hiyo kwa Simba ambayo ina majengo, viwanja na hata thamani ya nembo yake?
Mo: Nikuambie ukweli, Sh bilioni 20 ni fedha nyingi sana kwa anayeelewa biashara. Ningeweza kununua benki au ningeweza kununua klabu ya daraja la pili barani Ulaya, mfano kwa nchi kama Ureno. Lakini mapenzi ndiyo yamenisukuma kwenda Simba.

SALEHJEMBE: Nirudie kuhusiana na majengo, huoni yana thamani kubwa na huenda ungepaswa kuongeza?
Mo: Majengo yale pale Msimbazi thamani yake kupitia utafiti wao Simba ni Sh bilioni 3.5. Wewe utaangalia vingine vinavyobaki ni kiasi gani.
SALEHJEMBE:  Kama unaona Simba thamani yake ni chini, vipi utoe fedha nyingi zaidi?
Mo: Unapotaka kununua biashara kuna mifumo miwili, mmoja ni Valuation to Earn Ration. Unamuuliza mtu anaingiza kiasi gani kwa mwezi, labda anasema ni milioni 100. Halafu wewe unamlipa kwa miezi kumi ambayo ni Sh bilioni moja. Simba imekuwa ikiingiza hasara tu, ningesema niangalie hilo, huenda ningelipa kidogo sana lakini nia yangu ni kuendeleza na kuing’oa ilipo. Inatakiwa fedha nyingi zaidi kuliko ilivyo.

SALEHJEMBE: Umesema kuna mifumo miwili?
Mo: Yaa, mfumo wa pili ni Asset Valuation. Hapa unaangalia thamani ya mali ya unachotaka kukinunua, kwa Simba ukiangalia hilo bado ni chini sana. Hata kama ungeangalia ile nembo, nayo haiingizi faida. Mimi Mo naweza kuwa nauza maji kwa nembo ya Mo lakini hakuna faida kama siuzi, hivyo siwezi kusema eti lazima niuze kwa fedha ya juu maana mtu ananunua hasara.

SALEHJEMBE:  Uongozi wa Simba ulikubali kwenda kwenye mabadiliko, ilionekana ni shinikizo la wanachama. Lakini hawakusema wataufanya kwa muda gani, nini ushauri wako hapa?
Mo: Katika barua yangu niliyowaandikia, nimewaomba angalau mchakato uchukue miezi mitatu ili tuingie na kuanza kazi.

SALEHJEMBE:Ulisema utakuwa tayari kusaidia usajili, vipi utawapa kiasi gani?
Mo: Pia niliomba kukutana na viongozi na kamati ya utendaji. Usajili nitasaidia, mimi ni mwanachama wa Simba. Viongozi wengine hapo akiwemo Aveva, tulishirikiana pamoja kuisaidia Simba kuivua ubingwa Zamalek ikiwa timu bora Afrika mwaka 2003, hivyo wanajua kazi yangu na ninavyoweza kushirikiana na wengine. Kuhusu kiasi, inategemea tutakavyozungumza.

SALEHJEMBE: Umesema kuna viongozi hawataki mabadiliko, kina nani hasa?
Mo: Nilisema wanaongozwa na Evans (Aveva), lakini wengi tunafahamiana. Tena ni wachache tu na mmoja nimemwandikia ujumbe kumueleza nashukuru sana kuona ananipinga na hataki mabadiliko.

SALEHJEMBE: Kama mabadiliko yatafanyika, wewe ukaingia, unafikiri ndiyo kila kitu kwa Simba kwa maana ya mafanikio?
Mo: Simba ni klabu kubwa sana, nguvu yake ni watu, fedha ni chagizo la maendeleo. Mfumo bora ni chachu ya kusukuma na kuleta maendeleo. Nikiingia bado nitaendelea kuwa karibu na mashabiki na wanachama wa Simba ili tushirikiane kuingia kwenye mabadiliko ili kutafuta mafanikio.

SALEHJEMBE: Mwisho, unaona mafanikio ya matajiri kama Bakhresa upande wa Azam na Manji upande wa Yanga ndiyo yamekuvuta?
Mo: Labda umesahau, mimi nilikuwa Simba mwaka 2003, kipindi hicho wote hawakuwa wameingia kwenye mpira.

SALEHJEMBE: Vipi ni lazima uwe na asilimia 51 yaani majority share holder, shida nini hasa ukiwa chini ya asilimia 50?
Mo: Nikiwa chini ya asilimia 50 sina changu, kwanza kumbuka ninawekeza fedha Sh bilioni 20, si kitu kidogo ndugu yangu. Halafu kama nitakuwa sina uwezo wa uamuzi wa mwisho, itafikia siku mimi nataka fedha tupeleke kwenye vijana, wengine hawataki na sina nguvu, mambo yakiharibika, watu wataniuliza mimi. Hivyo ni lazima niwe nina uamuzi wa kufanya mambo kukimbilia kwenye mabadiliko na mafanikio.

SALEHJEMBE: Shukrani kwa ushirikiano.

Mo: Ahsante, karibuni wakati wowote.

2 COMMENTS:

  1. Welcome to CommHubb – you now own a piece of it!Just click the link below!
    http://www.commhubb.com/affiliate.php?ref=205643

    ReplyDelete
  2. saleh maswali ya kuzushi wamekupa kina kassim dewji,hawataki mabadiliko

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic