August 22, 2016


Ingawa niko mbali, lakini nyumbani ni nyumbani. Naendelea kufuatilia mambo mengi yanayotokea katika michezo au siasa. Na moja ambalo lilikuwa likinishangaza ni taarifa kwamba Wanayanga wanataka kuvamia nyumbani kwa Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali.

Nimesikia wanataka kuvamia kwake wamfanyie fujo, kisa ni uamuzi wake wa kuzungumza maneno ambayo yanaonekana kama yamemuudhi Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alitangaza kuamua kuachana na Yanga ingawa suala hilo, limekuwa na kizungumkuti.

 Akilimali naye ameamua kujihami, maana ni mtoto wa mjini. Tena safari hii ameamua kuwakaribisha wavamizi akisema anayetaka kupoteana na familia yake kwa muda usiojulikana, basi avamie kwake.

Inawezekana bado ningekuwa hapo nyumbani, ningeona si kitu kibaya sana. Lakini kwa kipindi hiki ambacho mimi nakutana na vitu vinavyonipa hamu ya kuona soka ya nyumbani inapiga hatua, halafu unasikia gumzo ni mzee Akilimali na mjadala ni upuuzi wa hali ya juu, inaniumiza sana.

Nakumbuka kuna mashabiki wa Simba, walikuwa na hasira kutokana na kufungwa kwa timu yao, wakavamia nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Hassan Dalali, wakajisaidia. Mwisho yeye aliwaonyesha busara na kuamua kuwapa maji wajisafishe, aibu kubwa. Baadhi ya watu hao, wako wanaomuona Dalali ni mmoja wa mashujaa wa Simba.

 


Wanaotaka kumvamia Akilimali kwa kipi hasa, kama amesema, kosa ni lipi? Kama anaamini tofauti, vipi avamiwe na nani anayetaka kuwaziba watu midomo na kwa nini? Labda isiwe ni Tanzania.
Lakini pia najiuliza, kila ambaye anampinga mzee Akilimali, yeye hajawahi kuwa na maoniyake tofauti na kuyatoa? Kwa nini mzee Akilimali asizidiwe kwa hoja badala ya kutumia ‘miguvu’ bila sababu za msingi!

 Watu wanazidi kupiga hatua kimaendeleo, Yanga ambao ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA kwa msimu uliopita, pia ni timu inayoaminika ina mashabiki wengi zaidi Afrika Mashariki, eti leo hii iko ‘bize’ na mzee Akilimali. Ajabu kabisa!

Lakini mzee Akilimali naye anaonekana ni mdhaifu, licha ya huo mkwara wake wa watu kupoteana na familia zao, lakiniyeye amewahi kufanya nini anachotaka kuzungumzia leo ambacho ni msaada hasa katika soka la kisasa ambalo linataka maendeleo yanayosaidia upatikanaji wa fedha?

Mzee Akilimali ana chuki na Manji? Alipomsema mbele ya wanachama, ni kinyongo? Anatumika? Kweli ni maoni ya dhati, kama ni hivyo, kabla ya kuingia kwa Manji msaada wake ulikuwa nini? Kuzungumza tu ili nayemaisha yaende, basi!

 Huyu mzee Akilimali ni nani kwenye Yanga, asipokuwepo kipi kitakosekana. Sasa anazungumza kwa maslahi ya Yanga au kuna mtu anamshika masikio asababishe kutoelewana ndani ya Yanga, ikiwa hivyo atafaidika nini au naye ni Yanga maslahi?


Yanga ni maskini, utajiri imeukalia. Yanga haina kitu kwa kuwa watu wake si wabunifu na wanaamini wakikaa kwenye kahawa na kupiga stori, huo ndiyo Uyanga. Dunia imepiga hatua elfu moja, sisi tumekaa palepale!


Akilimali kama anaona Yanga itapotea kupitia ofa aliyotoa Manji, basi naye atoe yake. Kama hawezi basi awasaidie Wanayanga, atafute mtu ambaye anaona ni sahihi.


Ana hofu Yanga kukodishwa miaka 10? Tena majengo, magari na uwanja vinabaki kuwa mali ya klabu. Hili ni jambo ambalo lilipitishwa kwenye mwafaka ambao yeye alishiriki kwamba klabu itakodishwa na timu itakuwa ikilipwa Sh milioni 100 kwa mwaka. Akilimali anajikausha vipi na hili?

Lakini hataki Yanga ibadilike, anataka iwe ileile, ili afaidike au anapata nini? Hataki kuwa ana hofu ‘duka’ litakuwa limevurugika au ana kingine?

Nafikiri, kuna haja ya kumsikiliza Akilimali, ameamua kufuta kauli yake, kawaombaradhi Wanayanga, ni mzee wao, wamsamehe. Lakini naye anapaswa kujifunza au ajiulize msaada wake umekuwa nini, kipi kimekuwa na faida?


Yanga haitakwepa uwekezaji. Wanachama walioamua ni wa Yanga, Akilimali au wengine wanaopinga walikuwa wapi, kwa nini hawakukataa pale? Hii ni harufu ya unafiki na kutaka kupindisha mambo. Mzozo huu ni kupoteza muda kwa pande zote mbili. 


Kikubwa ni kuangalia mambo ya msingi, kama mkataba wenyewe na faida zake na wapi upo sahihi au si sahihi.Kuendelea kulazimisha klabu hiyo isiingie kwenye mabadiliko ni sawa na kuzuia mvua kwa kujifunika na kipande cha gazeti.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic