August 22, 2016

Na Saleh Ally, Madrid
Baada ya kukaa siku kadhaa katika Jiji la Barcelona, niliamua kufunga safari kuja Madrid, mwendo wa takribani saa tatu kwa treni ya mwendo kasi wa kasi ya kilomita 393 kwa saa ikiwa imechanganya hasa.

Si karibu, ni umbali wa kilomita 621, lakini kasi ya treni, inafanya ionekane si safari ndefu sana. Hapa ndiyo makao makuu ya klabu bingwa Ulaya na tajiri kuliko zote duniani, Real Madrid.

Nilikueleza mengi kuhusiana na Barcelona, inawezekana yasiwe yote, lakini vizuri ukajua pia kuhusiana na uwanja maarufu duniani wa Santiago Bernabeu ambako Madrid wanayategemea zaidi mafanikio yao kupatikana hapa.

 





    Angalia Barcelona, Camp Nou iko katikati ya mji lakini kidogo kama vile ulivyo Uwanja wa Taifa. Santiago Bernabeu uko katikati kabisa ya mji, mfano Posta au Kariakoo kama ingekuwa ni Dar es Salaam. Hakuna nafasi kubwa sana ya mbwembwe na mambo yanaendelea.

Kama ilivyo kwa Barcelona, Santiago Bernabeu unaingiza fedha kutokana na watu wanaofika kuutembelea hapo kila siku kwa siku saba za wiki, ila niliona mashabiki hawakuwa wengi sana kama wale wa Camp Nou, inawezekana walizidi kwa asilimia 20 hadi 25.
   


 
Santiago Bernabeu ni uwanja unaoingiza watu 81,044, maana yake kwa Hispania unafuatia kwa ukubwa baada ya Camp Nou wa Barcelona ambao unaingiza watu 99, 354,.

Nilianza kwa kupanda hadi ghorofa ya mwisho kabisa, kutoka chini ni ghorofa nane ndiyo unalifikia jukwaa la mwisho kabisa, juu. Upandaji wake ni kutumia ngazi za mashine, baada ya hapo, ziara ikawa kuingia kwenye sehemu mbalimbali za makumbusho.


   
Ukiwa ndani utaona picha za vikosi vya zamani, kilivyo kikosi cha sasa, vikosi vilivyopata mafanikio hadi kikosi vya sasa. Hali kadhalika kwa wachezaji.

Kuna historia na maelezo ya wachezaji kupitia vipaza sauti, ukifika sehemu unataka kusikiliza au kuangalia basi unafanya hivyo mara moja.
     

  Kinachofurahisha zaidi, hata mechi za zamani, wanachukua sauti za watangazaji ambao walitangaza mechi zao. Unaweza ukasikiliza kwa ufupi hadi mechi za mwaka 1956.

Nembo ya klabu yao, ilivyoanza na kubadilika kwake hadi kufikia hapa ilipo. Pia kuna nafasi ya mashabiki kupiga picha na mastaa wao kama wapo.

Kama hiyo haitoshi, unaweza kuingia hadi sehemu mbalimbali. Mwisho ni kuuwezesha uwanja huo uliojengwa kwa kitita cha jumla ya euro milioni 17 (zaidi ya Sh bilioni 41), kuingiza angalau euro 23,000 (Sh milioni 56) au zaidi kulingana na siku ilivyo.

Lakini utaona namna watu hawa wanavyojua kwamba kweli soka ni biashara na si kama ilivyo nyumbani Tanzania, eti soka ni furaha. Hivyo watu wanaamini kwenye kufurahishana tu na kusahau kuwa wanacheza kwenye dimbwi la fedha huku wakilia umasikini.

Real Madrid wameyatengeneza makumbusho yao kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kwa mambo mengi yanayofanya uvutie. Mfano, picha za vikosi vya zamani, mfano mwaka 1959 na kadhalika, kulingana na historia fulani na watu wanapata nafasi ya kuona au kuwajua wachezaji.

Wana picha za video za wachezaji kipindi hicho, maelezo ya kutosha. Kila anayehitaji kujua kuna sehemu maalum anaweza kukaa na kusikiliza au kuangalia. Kama ambavyo ilivyo katika mechi zao za kihistoria, sauti za watangazaji, mfano Tanzania akina Abubakari Jongo au Abubakari Liongo zingekuwa zimehifadhiwa.

Makombe tangu miaka nenda rudi, yapo na maelezo yake. Mpangilio mzuri yalivyopangwa lakini nyota wake wa Galaticos na makombe ya uanasoka bora wa dunia, yamepangwa vizuri kabisa.

Utaona sura ya Zinedine Zidane, Ronaldo de Lima, Kaka, Luis Figo, Cristiano Ronaldo na wengine kibao. Wote sura zao zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na kuna kiboksi maalum mfano wa kombe walilokabidhiwa, lipo pale.

Utapita, mbele utapata nafasi ya kupiga picha na nyota wa humo ndani, mwisho unalipia takribani euro 2 hadi 4 ambazo ni kuanzia Sh 7,000 hadi Sh 9,000 au zaidi. Ukitoka hapo, unaingia kwenye duka la jezi na vifaa vingine ambalo limo ndani ya eneo hilo. Pale lazima utakuwa umejisikia raha au furaha ya ulivyoviona, utanunua jezi au vifaa vingine na mwisho unatokea uwanjani ili kupiga picha.

Kuna mengi huenda machache sijayazungumzia. Kikubwa hapa ni kukueleza kama ambavyo nilianza kuhusiana na Barcelona kwamba kwa klabu hizo kubwa, uwanja tu ni mtaji ambao unaweza kuwalipa wachezaji au wafanyakazi zaidi ya 1,000 ambao wameajiriwa na klabu kama Real Madrid.

Hii inaonyesha soka ni fedha hasa, lakini lazima uwe na mipango na ujitambue. Naendelea kuweka msisitizo, kwamba huku ninajifunza kwa niaba ya Gazeti la Championi na wasomaji wake.

Nawasisitiza Yanga na Simba wenye mitaji ya mashabiki, sasa waanze kuwatumia vizuri kwa kuwa wapo na hawawafaidishi, kwa viongozi wao bado wana yale mawazo ya uongozi wa enzi ya wale ambao walishindwa.

Nina mengi ya kukueleza, juzi nilirejea Barcelona kuona mechi kati ya Barcelona dhidi ya Real Betis kwenye Uwanja wa Camp Nou. Yapo ambayo nimejifunza na ningependa tushee tena.

Kabla nilikuwa kwenye ziara ndefu pia ya Jiji la Madrid. Nimepita kwenye ile minara miwili, mmoja hutumiwa na Real Madrid na mwingine Atletico Madrid wakati wa kushangilia na historia zao, nitakueleza pia.

Nimekwenda kwenye uwanja wa mazoezi wa Real Madrid. Kuna mengi kuhusiana na Madrid kuuza uwanja wa mazoezi na kuhama mjini. Pia ishu ya Messi na uamuzi wa kununua nyumba ilivyokuwa jirani yake. Unajua kisa ni nini? Endelea kufuatilia katika Gazeti la Championi Jumatano.

Bado sijajua mwelekeo kama nitarejea Madrid kuona mechi La Liga kati ya Atletico Madrid dhidi ya Alaves au nisafiri kwenda Milan, Italia kuangalia mechi kati ya AC Milan dhidi ya Torino ambako nimepata mwaliko wa nyota wa zamani wa AC Milan.

Acha nijaribu kubadili tiketi ikiwezekana, nitakujulisha. Hii ni Championi yako, NEXT LEVEL.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic