August 21, 2016

Timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefanikiwa kusonga mbele katika Hatua ya Tatu kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana ambayo itafanyika mwakani nchini Madagascar.


Serengeti ambayo katika mchezo wa kwanza wa Hatua ya Pili ya kuwania kufuzu michuano hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini, leo imefanikiwa kusonga Hatua ya Tatu ya kuwania kufuzu michuano hiyo baada ya kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 katika mchezo wa marudio uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.  

Kutokana na matokeo hayo Serengeti Boys imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1.








Ikishangiliwa na Watanzania wengi waliojitokeza uwanjani hapo Serengeti ilionyesha soka zuri na kufanikiwa kupata bao lake la kwanza katika dakika ya 33 kupitia kwa Mohamed Rashid Abdallah, bao ambalo liliwaamsha wageni na kufanya mashambulizi kadhaa lakini ambayo hayakuwa na faida.

Wasauzi waliendelea kupambana lakini bao lililofungwa na Muhsin Makame katika dakika ya 85 liliwamaliza nguvu wageni hao na kunyanyua shangwe nyingi uwanjani hapo ikiwemo hata kutoka kwa waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyekuwepo uwanjani hapo.


Bao hilo lilipatikana baada ya mfungaji kuunganisha krosi ya Mohammed Abdallah ambaye aliwatoka walinzi wa Sauzi na kupiga krosi nzuri iliyotua kwa Makame.

Katika mchezo huo, mchezaji wa Serengeti Boys, Ally Ng’anzi alipata kadi nyekundu katika hatua za mwisho kuelekea kukamilika kwa kipindi cha kwanza lakini hiyo haikupunguza nguvu ya Watanzania hao.


Mara baada ya ushindi huo, sasa Serengeti inasubiri kujua mpinzani wake ambapo ni kati ya Namibia au Congo ambao nao walitarajiwa kucheza leo, lakini tayari yenye nafasi kubwa kusonga mbele kati ya timu hizo ni Congo ambayo katika mchezo wa kwanza ilipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini.

Serengeti itaingia uwanjani kwa kuanzia nyumbani kukipiga na wapinzani wao hao katika Hatua ya Tatu mnamo Septemba 2016 kisha marudio yatakuwa Oktoba, mwaka huu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic