September 3, 2016


Kama unakumbuka katika zile mechi mbili za Yanga na Medeama ya Ghana? Kulikuwa na beki aliyeshiba, mwenye mwili mkubwa na mrefu kwelikweli akicheza beki ya kati ambaye muda wote Amissi Tambwe alipata shida, basi kwa taarifa yako tu, jamaa tayari ametua rasmi Azam FC na kuanza kazi.

Beki huyo anaitwa Daniel Amoah ambaye katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga alisababisha Tambwe kutolewa uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi wakati timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1. Yanga ilifungwa mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano nchini Ghana.

Amoah alitua nchini juzi akitokea kwao Ghana, Medeama walimuomba akawasaidie kwenye mechi za mwisho za makundi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe na MO Bejaia. Hata hivyo, timu hiyo imeshindwa kufuzu nusu fainali baada ya kufanya vibaya mechi ya mwisho.

Makamu Mwenyekiti wa Azam, Idrissa Nassor ‘Father’ ameliambiaChampioni Jumamosi: “Tunashukuru Amoah amefika. Alitua nchini usiku wa kuamkia jana (juzi) na leo (jana) alikuwa sehemu ya kikosi kilichoanza mazoezi baada ya mapumziko mafupi.”

Mbali na Tambwe, Laudit Mavugo wa Simba ambaye anaaminika kwa kusumbua ngome za ulinzi, atakuwa kwenye orodha ya kukumbana na gharika hilo la Mghana akicheza sambamba na Pascal Wawa wa Ivory Coast.

Kikosi hicho kinatarajia kuendelea na mazoezi leo na kundi la wachezaji wasiofikia 15 ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa.

SOURCE: CHAMPIONI.
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV