September 30, 2016

LUFUNGA (KULIA) AKIPAMBANA NA JOHN BOCCO WA AZAM FC
Wakati Simba ilipokuwa ikiendelea kujipanga kambini kwake mkoani Morogoro, ghafla kukaibuka mtihani wa mkanganyiko juu ya nani anastahili kuwa sahihi zaidi kuichezea Simba katika mechi yao dhidi ya Yanga kati ya Novaty Lufunga au Mganda, Juuko Murshid.

Awali iliaminika kuwa Juuko ana nafasi kubwa ya kuanza katika ‘first eleven’ ya Simba kwenye mechi hiyo itakayopigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar baada ya kupangwa kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya Majimaji na kumweka nje Lufunga, ikionekana kama anafanyiwa maandalizi ya mechi ya watani, kumbe ilikuwa tofauti.

Imeelezwa kuwa Lufunga aliwekwa benchi kutokana na kuwa na kadi mbili za njano ili kuepusha asipate kadi nyingine na kushindwa kutumika dhidi ya Yanga, lakini kiwango kilichoonyeshwa na Juuko kikabadili mawazo ya benchi la ufundi chini ya Mcameroon, Joseph Omog ikionekana kuwa Juuko yupo tayari kuizuia Yanga.

Hata hivyo, wakati benchi la ufundi likiendelea na maandalizi ya kuunda umoja wa Juuko na Mzimbabwe, Method Mwanjale, kiwango cha Lufunga nacho kikawa juu na kuanza kulikoroga benchi la ufundi la timu hiyo juu ya kipi ni sahihi.

Mmoja wa memba wa benchi hilo amelieleza Championi Ijumaa kuwa mipango ikabidi ibadilishwe na mara kwa mara kufanyiwa majaribio pacha ya Lufunga na Mwanjale dhidi ya Juuko na Mwanjale ili kupata kilicho bora lakini hata hivyo, ushindani wa pacha hizo umeshindwa kutoa majibu ya moja kwa moja.

“Bado haijaeleweka kati ya Juuko na Lufunga nani atapewa mikoba kutokana na ushindani uliopo ndiyo maana Omog mwenyewe alikuwa akiwabadilisha mara kwa mara katika mazoezi kuona kipi ni bora lakini imekuwa ngumu, kilichobaki ni maamuzi magumu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Ishu haipo kwa mabeki tu, hata pale kwenye mido bado kuna utata kwamba kutokana na uzito wa mechi, nani aanze kati ya (Said) Ndemla na Mzamiru (Yassin), ushindani ni mkubwa.”


Alipotafutwa Lufunga kuzungumzia suala la kadi, alisema hawezi kulitolea ufafanuzi labda meneja wa timu, Musa Mgosi. Alipotafutwa Mgosi naye, simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV