Ligi Kuu Tanzania Bara ndiyo kwanza bado ipo katika hatua za awali, habari ya mjini ni kuwa kuna wababe wawili wa ligi hiyo wanatarajiwa kukutana kesho, vijana wa mjini wanatamba kuwa kesho Jumamosi ‘Hawataki mambo ya kijinga’ kwa kuwa wao wanachotaka ni kuona soka zuri na mbabe mmoja anapata kipigo.
Wababe hao ni Yanga na Simba, ambapo timu moja itakayoshinda lazima itaondoka na ‘kijiji’ kwa asilimia kubwa pale kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo ndipo kutakapopigwa kipute hicho, wale watakaofungwa itakuwa ‘aibu yao wenyewe’ lakini mchezo ukiwa sare basi matokeo hayo yanaweza kupunguza utamu wa tambo mitaani.
Kuelekea mchezo huo, tayari presha ni kubwa, taarifa ikufikie kuwa bilionea wa Simba, Mohammed Dewji 'MO' ambaye yupo mbioni kununua hisa kwa asilimi 51 klabuni hapo ili kuwa mmiliki wa klabu hiyo, ametumia shilingi milioni 78 kuwalipia mishahara wachezaji, benchi la ufundi na sekretarieti ya timu hiyo.
Hatua hiyo imekuja, saa chache kabla ya mchezo huo ikiwa ni moja ya njia za kuongeza hamasa kwa timu yake na kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kuisaidia timu hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara amesema uongozi wa Simba umemshukuru mlezi wao Dewji kwa kuanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.
"Ukizingatia klabu kwa sasa haina mdhamini, naamini uwekezaji huo ni chachu ya kuwarejeshea furaha Wanasimba.
"Tunawaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi Taifa kuishangilia timu yetu kwa kuwa tunaamini mchezo huo utakuwa ni mwendelezo wa furaha kwa wanachama na mashabiki wetu kote nchini baada ya ushindi wa mfululizo katika mechi zilizopita za ligi kuu," alisema Manara.
Kuelekea mchakato wa kununua hisa, MO alisema atanunua hisa hizo kwa Sh bilioni 20, ambapo kinachofanyika sasa ni mabadiliko ya kutoka kwenye mfumo wa wanachama na kuwa kampuni.
0 COMMENTS:
Post a Comment