September 3, 2016

KIKOSI CHA MBEYA CITY, MWAKA JANA.

Kwenye wikiendi hii ni nafasi ya pekee kwa Mbeya City kuongoza Ligi Kuu Bara kwani timu nyingine zenye pointi nne hazitocheza mechi zao hadi hapo baadaye.

Azam FC inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi nne sawa na Simba iliyo nafasi ya pili, Ruvu Shooting ya tatu, Prisons ya nne na Mbeya City ya tano.

Timu hizo zote zimecheza mechi mbili ambapo zimeshinda moja na kutoka sare moja, lakini ni Mbeya City pekee itakayoshuka uwanjani wikiendi hii ambapo leo Jumamosi itacheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Isipofungwa Mbeya City, yaani ikishinda au kutoka sare itakuwa imekaa kileleni ikikumbuka msimu wake wa kwanza katika ligi hiyo miaka miwili iliyopita.
Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri raia wa Malawi alisema: “Kikosi changu kipo vizuri kwa ajili mchezo huo na ninaamini tutafanikiwa kuongoza ligi tangu ilipoanza msimu huu.”

Naye Kocha wa Mbao FC inayoshika nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi moja, Ndairagije Etiene, alisema: “Ushindi katika mechi hiyo ni lazima kwani tupo katika nafasi mbaya, tutaingia uwanjani kupambana ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri yatakayotupandisha juu kwenye msimamo wa ligi.”

Katika michezo mingine ya ligi hiyo leo Jumamosi, kwenye Uwanja wa Kaitaba wa mjini Bukoba, Kagera Sugar itavaana na Mwadui FC,  Majimaji FC itapambana na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Majimaji, Songea) wakati JKT Ruvu itapambana na African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.


Kesho Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ambapo Stand United itacheza na Toto Africans ya Mwanza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV