September 30, 2016
Na Saleh Ally
OKTOBA 20, 2013, Yanga na Simba zilikuwa uwanjani katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Hadi mapumziko, Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 3-0.

Mashabiki wa Yanga, waliamini msimu wa 2013-14, ndiyo ulikuwa wakati mzuri kwa wao kulipiza lile deni la kufungwa mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa Mei 6, 2012 kwenye uwanja huo.

Wengi wao waliimba kwa furaha huku wakiwaonyesha vidole mashabiki wa Simba vikiashiria kipigo cha mabao matano au sita kinafuatia.

Lakini hadi dakika 90 zinakamilika, matokeo yalikuwa 3-3 huku Simba ikionekana kuwa na nafasi baada ya beki wake Joseph Owino kupoteza nafasi ya kufunga bao la nne.

Waliogeuza mchezo huo ni makinda wawili, William Lucian ‘Gallas’ na Said Hamis Ndemla. Tena walifanya hivyo mbele ya wakongwe kama Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na wengine ambao walionekana kuwa hawakamatiki.

Pamoja na sare hiyo, Yanga walitoka uwanjani wakiwa wamelowa, hawana hamu. Idadi kubwa ya mashabiki wake walizimia na wengi walikuwa wakilaumu. Hofu yangu, Simba wasipoangalia, hili linaweza kuwatokea.

Ukipata nafasi ya kuwasikia wengi wanazungumzia mechi ya watani Yanga na Simba inayopigwa kesho Jumamosi, asilimia 80 sasa wanazungumzia Yanga kufungwa na asilimia 80 wanaamini Simba Kushinda. Wako Yanga wameishakata tamaa na Simba, wanaamini wao hawashikiki.

Wengi wanazungumzia kwamba Yanga imeishapoteza mechi moja na wanaamini huenda Yanga wamechoka sana kutokana na kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Shirikisho hadi hatua ya robo fainali, hivyo hawana lao.

Hisia zinaweza kuwa sahihi, lakini takwimu hupewa nafasi zaidi kuliko hisia za moyo tu. Bado hata takwimu wakati mwingine hufeli kwa kuwa msema kweli katika mchezo wa soka, mara nyingi ni dakika 90. Kila dakika 90 za mchezo, zinajitegemea.

Ukitazama  msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba inaongoza ikiwa na pointi 16, inafuatia Stand United ina pointi 12, Yanga ina 10 sawa na Azam FC. Hizi ni timu zinazofundishwa na makocha kutoka nje ya Tanzania.

Kitakwimu, hupati tofauti kubwa sana. Yanga inazidiwa pointi sita na Simba, lakini ina mchezo mmoja kibindoni. Mwendo wa Simba ni mzuri lakini kumbuka pamoja na kuwa na timu yake nzuri, ilishindwa kufunga bao hata moja katika mechi dhidi ya JKT ambayo bado si timu bora zaidi katika msimu huu.

Yanga pia ilibanwa na kuambulia sare ya bila kufungana na Ndanda FC pale Nangwanda Sijaona. Utaona kwamba bado timu hizi zinalingana na zinaweza kuingia kwenye sare, kitakwimu hii inaonyesha sare ni matokeo yanayoweza kupatikana kesho.

Tofauti kubwa kati ya timu hizo ni kwamba, Yanga imepoteza mechi moja dhidi ya Stand United na hii ndiyo sehemu nzuri ya kujifunza kwa kuwa, Yanga imepotezea mechi hii mkoani, kwenye uwanja mbovu kama ilivyopata sare yake dhidi ya Ndanda.

Haina sare wala kupoteza Uwanja wa Taifa.
Sare ya Simba ni kwenye Uwanja wa Taifa ambao ni mzuri na timu hasa hizi zinazofundishwa na makocha wa kigeni, zinaweza kucheza mpira zinaoutaka.

Takwimu zinaonyesha katika mechi sita, Simba imefunga mabao 12 na imefungwa mawili tu. Yanga katika mechi tano imefunga mabao nane na kufungwa moja tu. Hapa ni takwimu zisizokuwa na tofauti kubwa sana hadi kufikia kuamini timu moja lazima iifunge nyingine.

Simba imeshinda mechi tano, Yanga imeshinda mechi mbili, kila upande una sare moja. Hakuna ubishi hapa, kwamba bado Simba inaonekana kuwa bora angalau kwa 60% kwa 40% za Yanga, lakini hakuna tofauti kubwa inayoweza kukupatia uhakika.

Uhakika ni dakika 90 kwa kuwa bado Yanga wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri zaidi kwa kuwa wana kikosi chenye wachezaji waliozoeana zaidi ya Simba. Wengi wao wamecheza mechi hiyo ya watani kuliko wale wa Simba.

Yanga ina wachezaji ambao hawatakuwa na hofu tena na wanajua nini wafanye. Wameifunga Simba mara mbili wakiwa pamoja. Simba ina wageni ambao itategemea watacheza vipi, kwa kiwango cha juu au watapata hofu kwa kuwa mechi ya watani, mchezaji anatakiwa kujipanga kweli.

Ukiangalia vizuri utagundua mechi ya kesho ubora wake upo kwenye uchangaji wa karata kuanzia wakati wa maandalizi na ndani ya dakika 90. Kuangalia mwendo wa Simba ulivyo na kupitisha kwamba ni lazima iifunge Yanga ni kosa jingine kubwa, huenda litaongeza idadi ya watakaoshituka au kupoteza fahamu kama mambo yakiwa tofauti.

Yanga walichanganywa na kutangulia na mabao 3-0 hadi mapumziko lakini dakika 45 zilizobaki, zikatoa majibu tofauti ambayo kati ya watu zaidi ya 60,000 waliokuwa uwanjani, hakuna aliyeweza hata kuwaza inaweza kuwa hivyo.

Sasa ni vizuri kukubali, soka si mchezo unaotabirika. Na kama inawezekana kubashiri, basi tahadhari lazima ikae katikati, Yanga bado wana watu hatari wanaoweza kuamua matokeo, kocha mzuri anayeweza kubadili gia.


Yeyote anaweza kufungwa na kikubwa kinachotegemea ni yule atakayetumia nafasi na kupunguza makosa, atafanya vizuri. Atakayevuruga na kukosea sana, hasa makosa ya hovyo, ataadhibiwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV